Na John Mapepele
Serikali imesema zoezi la kuhama kwa hiari wananchi wanaoishi kwenye Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Msomela mkoani Tanga litakamilika Machi 30 mwakani ili kupisha uhifadhi wa raslimali katika eneo hilo.
Kauli hiyo ameitoa Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa leo Agosti 21,2023 kwenye kikao baina ya Wizara na Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi,Maliasili na Utalii wakati kamati hiyo ikipokea na kujadili taarifa za serikali kuhusu utendaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania(TAWA) na utekelezaji wa zoezi la hiari la kuwahamisha wenyeji kutoka ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.
“Naomba kutoa taarifa kwa kamati yako mwenyekiti kuwa taratibu zote za uhamishaji wananchi kwa hiari awamu ya pili kutoka kwenye hifadhi ya Ngorongoro zimekamilika na kwamba Serikali imeshatoa fedha kwa ajilin ya zoezi hilo hivyo zoezi hilo litafanyika kama lilivyopangwa”. Amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Amewaelekeza watendaji wote kuhakikisha kuwa wanasimamia zoezi hilo kwa weledi, wakitanguliza uzalendo huku akionya kwa mtendaji yoyote ambaye anakwenda kinyume atachukuliwa hatua za kisheria.
Akizungumzia kuhusu utendaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania(TAWA) na namna wizara ilivyojipanga kukabiliana na na changamoto za Wanyama waharibifu Mhe. Mchengerwa amesema wizara yake inakwenda kuwekeza katika teknolojia ya kisasa ili kudhibiti wanyama waharibifu.
Aidha amesema tayari Wizara katika kipindi kifupi imeshafanya marekebisho makubwa ya sheria na kanuni kadhaa za sekta zake zote ili ziendane na hali halisi ya sasa.
Amefafanua kuwa changamoto nyingi zinazoikabili baadhi ya masuala ya sasa ikiwa ni pamoja na wanyama waharibifu kama Tembo ni kutokana na matatizo ambayo yalitengenezwa kwa kufanya jambo moja bila kuzingatia masuala mengine kama mipango ya matumizi bora ya ardhi.
Amemtaka Naibu Katibu Mkuu Kamishna Benedict Wakulyamba ambaye ndiye msimamizi wa uhifadhi katika wizara kuhakikisha changamoto ya wanyama wahalibifu inapata suluhisho la kudumu.
Pia Mhe. Mchengerwa amesema kwa sasa Wizara imeshatoa ridhaa ya wawindaji wenyeji kufanya uwindaji ambapo pia wametoa ridhaa ya kufanya uwekezaji wa zoo za Wanyama.
“Tumeshaandaa block tatu upande wa kaskazini ambazo zitakuwa chini ya Serikali na tunaendelea kutengeneza miundombinu ili iwe bora na kutoa fursa kwa watu kuwinda”. Ameongeza Waziri Mchengerwa
Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe.Timetheo Mzava kwa niaba ya Kamati yake ameipongeza Wizara kwa kazi nzuri inayofanya katika kipindi hiki huku akiitaka kuongeza juhudi za kukabili changamoto zinazowakabili wananchi hususan Wanyama waharibifu.
“Sote tumeona pamoja na kazi nzuri na mikakati mliyojiwekea tunawapongeza sana na tunataka mfanye vizuri zaidi”. Amesisitiza Mhe. Mzava wakati akikifunga kikao hicho
Aidha amesema katika siku za nyuma wizara ilikuwa haifanyi vizuri ukilinganisha na kipindi hiki kwa kuwa ilikuwa inachukuwa muda mrefu katika kufanya maamuzi
“Maamuzi yamekuwa yanachelewa sana, vitu kama vipepeo vya amani, suala la kusafirisha viumbe hai na mambo mengine yamekuwa yakichukua muda mrefu” ameongeza
0 Comments