Na Mwandishi Wetu, Arusha
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limewatembelea wajasiriamali ambao wanashiriki Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayofanyika katika Viwanja vya Themi- Njiro, jijini Arusha ili kujua changamoto zao sambamba na kuwapa elimu ya kuthibitisha ubora wa bidhaa zao.
Msisitizo wa TBS kuwahimiza wajasiriamali hao kujitokeza kuthibitisha ubora wa bidhaa zao unaotokana na huduma hiyo kuwa inatolewa bure kwao, kwa kuwa Serikali inatenga kati ya sh. milioni 150 hadi 200 kila mwaka kwa ajili ya kuwahudumia.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho hayo jana, Meneja Uhusiano na Masoko wa TBS, Gladness Kaseka, alisema hadi sasa zaidi ya wajasiriamali wadogo 600 kutoka mikoa mbalimbali wamepata leseni chini ya mpango huo bure.
Alisema TBS ipo kwenye maonesho hayo tangu Agosti 1 yalipoanza hadi Agosti 8, mwaka huu (leo) hasa kwa kuzingatia kwamba shirika hilo ni wadau wakubwa, ikizingatiwa lengo lao moja wapo ni kuwezesha biashara.
"Kwa hiyo tupo kwenye viwanja hivi kwa ajili ya kusikiliza changamoto, kuzitatua na kutoa elimu na kuwapa msaada wadau wetu kuhusiana na huduma mbalimbali za Shirika," alisema Kaseka.
Kwa mujibu wa Kaseka, miongoni mwa huduma hizo ni pamoja na usajili wa bidhaa na majengo ya chakula na vipodozi, leseni ya kutumia alama ya ubora na msaada wa kitaalam kwa wanaosafirisha bidhaa nje ya nchi pamoja na umuhimu wa kusoma taarifa za kwenye vifungashio hususani kujua muda wa mwisho wa matumizi wa bidhaa husika.
Kaseka alitoa wito kwa wateja na wananchi kutumia fursa hiyo kwa kutembelea banda la TBS lililopo ndani ya viwanja hivyo na watakaoshindwa wasisite kuwasiliana na TBS kupitia kituo cha huduma kwa wateja.
Maonesho hayo yaliyoanza rasmi tarehe 01/08/2023 na kufunguliwa na Spika wa Bunge wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Zubeir Ali Maulid, yamebebwa na kauli mbiu isemayo; " Vijana na wanawake ni msingi imara wa mifumo endelevu ya chakula."
0 Comments