Mkuu wa Wilaya ya Monduli Mhe. Joshua Nassari (Kushoto) akipata maelezo kuhusu mbegu za Ngwara NM-D19 na NM-D20 zilizoboreshwa kutoka Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu ya Kilimo ya Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Endelevu Bi. Monica Nakei katika maonesho ya 29 ya nanenane Kanda ya Kaskazini viwanja vya Themi Njiro, Arusha
Mbegu za Ngwara NM-D19 na NM-D20 zilizoboreshwa kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela.
Na Mwandishi Wetu - Arusha
Wakulima wameshauriwa kutumia mbegu za Ngwara, NM-D19 na NM-D20 zilizoboreshwa kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela ili kuzalisha mazao bora kwa wingi.
Wito huo umetolewa na Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu ya Kilimo Endelevu, Bi. Monica Nakei kutoka katika Taasisi hiyo katika maonesho ya 29 ya Nanenane Kanda ya Kaskazini yanayoendelea kwenye viwanja vya Themi Njiro, jijini Arusha.
“Mbegu hizi za Ngwara NM-D19 na NM-D20 ni matokeo ya tafiti iliyofanywa na taasisi yetu ambayo inauwezo wa kuzalisha kwa wingi, kustahimili ukame na ladha nzuri kwa chakula . “ Alisema Bi. Monica Nakei
Anazidi kueleza kuwa mbegu hizo zilizoidhinishwa na Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI), zina faida kubwa kwa kuwa na uwezo mkubwa wa kurutubisha udongo, kuhifadhi maisha ya viumbe hai muhimu kwenye udongo, kusaidia kupunguza na kuzuia mmomonyoko wa udongo pamoja na kuhifadhi maji na mbolea kwenye udongo.
Bi. Monica anaeleza sifa nyingine za Ngwara inaongeza uzalishaji wa maziwa kwa akinamama wanaonyonyesha, kuharakisha uponyaji wa vidonda pamoja na kusaidia katika kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo kansa.
Mbali na faida hizo za kiafya, zao hili hususani Ngwara Nyeusi lina soko kubwa katika nchi ya jirani ya Kenya, hivyo ni fursa kubwa katika kuinua uchumi wa wakulima na nchi kwa ujumla.
0 Comments