Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ameipongeza Taasisi ya WAMA kwa kutoa fursa ya elimu kwa watoto wanaotoka katika mazingira magumu na yatima kupitia shule ya sekondari ya Wama Nayakama iliyopo wilayani Kibiti Mkoa wa Pwani na WAMA Sharaf iliyopo Mkoani Lindi.
Waziri Mkenda ametoa pongezi hizo alipotembelea shule ya Wama Nakaya Kibiti kuona maendeleo ya elimu kwa shule hiyo ambapo amesema kinachofanywa na Taasisi hiyo ni kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha elimu bora inatolewa na kwa usawa.
“Mafanikio ninayoyaona wazi katika shule hii bila kusema ni fursa ya masomo kwa watoto hawa, pengine wasingepata fursa ya kusoma lakini Taasisi ya WAMA inawasaidia kwa asilimia 100 na huu ndio mwelekeo wa Serikali kuhakikisha hakuna anaebaki kwenye mfumo wa elimu, sasa ni lazima tuunge mkono juhudi hizi, tuendelee kufanya kazi na ninyi,”amesema Prof. Mkenda
Amesema Rais Samia amejitahidi kuhakikisha watoto wa kitanzania wanapata elimu kwa usawa kwa kuondoa ada kuanzia elimu ya Awali hadi kidato cha sita, kuongeza mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na sasa kuleta mikopo kwenye Vyuo vya kati.
“Pamoja na hayo yote yaliyofanyika, Serikali inajitahidi kwenye mgawanyo wa rasilimali kila mahali kuna miradi ya elimu inaendelea lengo ni kuhakikisha hakuna mtoto anachwa kwenye mfumo wa elimu,” ameongeza Waziri Mkenda
Amesema Serikali pamoja na kuongeza mikopo inatoa Samia Scholarship kwa wanafunzi wanaofanya vizuri sana kidato cha sita katika masomo ya sayansi na kuingia Chuo Kikuu kusoma Sayansi, Hisabati Tehema Uhandisi au Elimu tiba hivyo amewaasa wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili kufaulu kwa alama za juu ili waweze kupata ufadhili huo.
Kwa upande wake Afisa Elimu wa Taasisi ya WAMA Mohamed Zome amesema Shule hiyo ilianza mwaka 2010 na kwamba inachukua wanafunzi wanaotoka katika mazingira magumu nchi wote wakifadhiliwa na Taasisi hiyo.
Amesema Shule hiyo kwa sasa ina wanafunzi 292 na inatoa michepuo yote. Akizungumzia ufaulu wa shule hiyo Zome amesema shule hiyo inafanya vizuri na kwamba katika matokeo ya kidato cha sita wanafunzi 54 wamefaulu kwa divisheni I-III kati ya wanafunzi 59 waliofanya mtihani wa Taifa wa kuhitimu kidato cha sita.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi katika shule hiyo wamefurahia ujio wa Waziri wa elimu katika shule hiyo na kuahidi kufanya vizuri katika masomo yao ili waweze kupata samia Scholarship.
0 Comments