Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt Ashatu Kijaji(Mb.) amewasihi Watanzania kuuza ziada ya chalula na kubakisha chakula chakutosha hadi msimu ujao ili kutokununua chakula hicho kwa bei kubwa zaidi wakati ujao.
Vilevile, amewashauri Wafanyabiashara wa nafaka kununua nafaka kwa wingi zinapopatikana na kuzisambaza kwenye maeneo zinapohitajika ili kuwasaidia wananchi kununua chakula mapema kwa bei nafuu ukilinganisha na miezi ijayo ya msimu wa kilimo.
Waziri Kijaji ameyasema hayo akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Lugano Wilson na Katibu Tawala wa Mkoa huo Kamishna Dkt. Mussa Ali Mussa alipokuwa akitoa Taarifa ya tathimini ya Mwenendo wa Bei za Bidhaa Muhimu Nchini kwa Mwezi Septemba 2023 katika Mkutano wa Waandishi wa Habari uliofanyika Mkoani Morogoro 15/09/2023
Aidha, Waziri Kijaji ametoa rai kwa wazalishaji wa bidhaa zote za viwandani kuongeza jitihada za kuzalisha bidhaa kwa kuzingatia ubora unaohitajika sokoni na kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa ili kukabiliana na kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali nchini.
Vilevile, Waziri Kijaji amebinisha mwenendo wa bei za bidhaa muhimu kwa Septemba 2023 imeonesha bei ya mazao ya mahindi, unga wa mahindi, maharage, unga wa ngano imepungua, viazi mviringo. Sukari himilivu, Mafuta ya kupikia na mchele imeongezeka kidogo, wakati bei ya vifaa vya ujenzi kama saruji, nondo na bati imeongezeka kidogo.
Aidha, amewatahadharisha wafanyabiashara kuwa makini na kujiridhisha kupitia Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania kuhusu Makampuni ya Wakala wanatoa matangazo ya kuandaa safari za kibiashara nje ya nchi bila kufuata taratibu na kuwalaghai kutoa kiasi cha fedha kama sehemu ya gharama za kujisajili ili waweze kushiriki katika ziara hizo.
Kwa upande wa mikataba ya biashara baina ya Nchi na Nchi (bilateral), Kikanda na Kimataifa, Dkt Kijaji amebainisha kuwa Watanzania wanaweza kuuza bidhaa na huduma katika masoko ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC); Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) pamoja na Nchi kama vile India, Japan, Marekani (AGOA) na China.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima amewashauri wakulima na wazalishaji nchini, kuutumia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ili waweze kupata manufaa na kuongeza tija ya mauzo ya mazao na bidhaa zao kila mkoa nchini.
0 Comments