Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Agri Thamani Mhe. Neema Lugangira amezindua Kampeni ya "Pika kwa Gesi, Tunza Mazingira" inayolenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo aliyotoa Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan wakati wa Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia lililofanyika tarehe 1 Novemba 2022, Dar es Salaam.
Kampeni ya Pika kwa Gesi, Tunza Mazingira inaratibiwa na Ofisi ya Mbunge Lugangira kupitia Neema Na Maendeleo na Shirika la Agri Thamani ambalo Mbunge Lugangira ni Mwanzilishi wake. Kampeni hii imeanzia Wilaya ya Bukoba Mjini ikifuatiwa na Wilaya ya Muleba alafu itafika maeneo mengine ndani na nje ya Mkoa wa Kagera kulingana na uwezeshwaji utakaopatikana.
Kupitia Uzinduzi wa Kampeni ya Pika kwa Gesi, Tunza Mazingira; Mhe Neema Lugangira ametoa jumla ya Mitungi 300 ya Gesi kwa Viongozi wa Makundi Mbalimbali, Wajasariamali, Mama Lishe na Watu Mashuhuri katika Wilaya ya Bukoba Mjini
Mhe Neema Lugangira amewashukuru Wizara ya Nishati kwa kuwapa Semina Wabunge kuhusu umuhimu wa kuhamasisha nishati safi ya kupikia na uwezeshwaji uliofanikisha uzinduzi huu.
Aidha, Mhe Lugangira anamshukuru sana Bi. Jamilla Haroub Juma, Mratibu wa REA Bukoba na Bw. Masota Daudi Mafuru, Afisa Masoko Oryx Gas Mkoa wa Kagera & Geita kwa ushirikiano mkubwa waliompatia.
Kwa kuhitimisha, Mhe Neema Lugangira anakaribisha Wadau kumuunga mkono kufanikisha Kampeni ya Pika kwa Gesi, Tunza Mazingira ili kuweza kufikia Makundi mengine mengi kwenye jamii kwa lengo la kulinda afya za wakina mama, kutunza mazingira na kuepusha madhara ya mabadiliko ya tabia nchi, mambo ambayo yatapelekea kuimarisha Lishe Bora.
0 Comments