Na Said Mwishehe,
SIMU iliyopigwa na Rais Samia ya kuniita Ikulu binafsi imenishutua sana, na zipo sababu kadhaa zilizofanya niogope.
Ilipigwa simu ngeni kupitia namba yangu ya 0713833822, ilipopigwa mara ya kwanza sikupokea kwasababu ilikuwa ni namba ngeni, baada ya kupita dakika tano ikapiga tena namba ile ile, nikasema ngoja niipokee.
Nikachukua simu yangu ya kitochi na kubonyeza kile kitufe cha kupokelea simu, ile napokea tu nikasikia sauti ikinisalimia kwa kusema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania....nikajibu kazi iendelee lakini nikawa najaribu kuisikiliza sauti.
Kwa bahati nzuri wakati natafakari nani anapiga, akajitambulisha kwamba "Naitwa Rais Samia Suluhu Hassan " alivyojitambulisha tu nikaona mwili kama umekufa ganzi, nilikuwa nimesimama nikatafuta tofali nikakaa ili nisikilize anataka kuniambia nini.
Nilichokifanya nikamsalimia kwa kumpa heshima yake, Shikamoo Mama na Rais wangu mpendwa.Akaitikia na kisha kuzungumza maneno mafupi tu , "Nakuhitaji uje Ikulu nina mazungumzo na wewe Said Mwishehe."
Hakika nilijikuta moyo unaenda mbio, mapigo ya moyo yakaongezeka kama vile nimekimbizwa na wasiojulikana.Lakini nikajipa moyo na kumjibu Rais Samia nimepokea maelekezo yako.Nikamuuliza , nije lini akasema uje kesho saa tano kamili asubuhi Ikulu ya Dar es Salaam.
Nakumbuka alipiga simu saa nane mchana na baada ya simu yake kukata nikaanza kutafakari kuna nini ambacho Rais ananiitia Ikulu? Mbona sina cheo, sina ukubwa, sio maarufu, sio mkosefu, sina tabia za hovyo.
Yaani najiuliza hivi Rais namba yangu amepewa nani? Mbona sina anayenijua, mbona sina urafiki na mkubwa yoyote? Hivi Rais Samia ananiitia nini mimi, mtu niliyekapuku na sina mbele wala nyuma.
Niliwaza mambo mengi sana, nikaanza kujifanyia uchunguzi binafsi ili nitafute kama kuna kosa nimelifanya katika nchi yangu, nikakuta sina, nikajaribu kuwaza labda nimemkosea lakini najikuta sijamkosea Rais wangu, kwanza nampenda, namheshimu na hakika sina shaka naye hata kidogo.
Nikasema wala isiwe tabu, kesho nitakwenda kama alivyotaka.Nitakwenda kumsikiliza na niko tayari kupokea maoni na ushauri wake.Lakini usiku niliamua kutenga muda wa kumuomba Mungu safari ili yangu ya kwenda kuonana na Rais Samia ikawe yenye heri.
Jua lilipochomoza kama kawaida ya binadamu wengine wote ratiba ya asubuhi ikachukua nafasi yake lakini muda wote nawaza leo ndio siku ya kukutana na Rais Samia.
Kwangu ni Majohe kwa Ngozoma na barabara yetu ni ya vumbi ingawa kuna kipande cha mita 100 hivi ndio kimewekwa lami juzi juzi tu hapa, hivyo nikajipanga , Rais akinipa nafasi tu ya kusikiliza shida yangu basi nitamuomba atusaidie kutuwekea lami kutoka Pugu Sekondari kupita Majohe kwa Ngozoma hadi kwa Mpemba, ndio kilio chetu kikubwa na ni cha muda mrefu.
Niliamua kuondoka nyumbani mapema ili nisichelewe Ikulu kama ambavyo Rais Samia alivyonipa taarifa yake, niliamua kuvaa suruali yangu , shati na kuweka na tai shingoni.Naenda kukutana na Rais, tena kwa mualiko wake .
Saa nne na nusu nikawa niko nje ya geti kubwa la kuingia Ikulu ambalo linatazamana na Bahari ya Hindi, wakati huo naendelea kujipa ujasiri na nikawa navuta vuta muda ili zikiwa zimebakia dakika 10 niende kujitambulisha pale getini.
Hata hivyo nikawa najiuliza mwenyewe hivi hawa ndugu hapa getini watakuwa na taarifa za ujio wangu.Lakini haikunipa shida sana, nimeitwa na Rais Samia, hofu ya nini.Nikajua wakiniuliza nitawaeleza sababu za kwenda Ikulu.
Muda ulipofika nikasogea kwa walinzi, ilikuwa saa tano kasoro dakika 10, wakati naanzaa kujitambulisha nikaona watu kama wanne hivi wakiwa na Rais Samia wanakuja katika geti nililokuwepo.Rais alipofika akaniuliza ni Said nikamjibu ndio, akasema karibu Ikulu, nimekuja kukupokea mwanangu.
Nilipigwa na butwaa lakini nikajipa nguvu na kumjibu ahsante Mheshimiwa Rais, nikamsalimia na kisha tukaanza kuelekea ofisini kwake pale Ikulu, yeye kulia na mimi kushoto na walinzi wake wakiwa nyuma kama hatua tano.
Akili kwangu nikawa najiuliza tu hivi kuna jambo gani ameniitia, Rais anataka kuniambia nini? Wakati huo tunakwenda na ananiuliza salamu za nilikotoka, naendeleaje.Naitikia lakini kichwani naendelea kutafakari.
Ukweli nikiri, kwangu kupokelewa na Rais Samia nilijisikia moyo wangu kuwa na amani tele, basi bwana tukaenda mpaka ofisini kwake pale pale Ikulu, lakini baada ya kunikaribisha kwenye kochi zuri ambalo kwangu nadhani bila yeye nisingekaa kwenye kochi kama lile, kochi la Ikulu mtaani unalikuta kwa nani.Kochi linanesanesa na ukikaa linakupokea.
Nilipokaa na yeye akakaa kwenye kochi lake, lakini kabla ya kuniambia alichoniita aliwataka walinzi wake waondoke, hata mlinzi yule ambaye namuonaga tu kwenye luninga anasimamaga nyuma ya Rais naye alimuondoa.
Tukabaki mimi na Rais Samia, wakati wale walinzi wanaondoka nikasema kimoyomoyo Rais anataka kuniambia nini?Kwanini tubaki wawili, kuna mazungumzo gani?
Walivyoondoka Rais akasimama na kwenda kufunga mlango, lakini wakati ananyanyuka akaniambia nisiwe na hofu, niwe huru ameniita kwa nia njema na hakuna jambo la kushangaza kuniita Ikulu kwani amewaita watu wengi na kwa nyakati tofauti.
Alipofunga mlango akarudi kwenye kochi lake na kunikaribisha tena wakati huo akimimina juisi kwenye glasi yake na kisha akaniwekea na mimi.Kwangu ilikuwa ni ajabu, sikutarajia kama nitapata mapokezi ya aina hiyo na sio mapokezi tu wala haikuwa kichwani kama kuna siku Rais wa nchi ataniita Ikulu kuzungumza na mimi.
Basi nikachukua juisi yangu ya parachichi nikapiga fundo moja na kumeza kwa upoleee, inapita kooni huku naisikiliza.Hata kama ingekuwa wewe ungefanyaje , juisi ya Ikulu halafu unawekewa na Rais wa nchi.
Kwa wakati ule kichwani kwangu moja kwa moja nikamuweka Rais Samia katika sura tatu, kwanza kama Rais wangu katika nchi, pili kama Mama mlezi mwenye upendo kwa mwanaye na tatu nikamuona ni Rais, ni mama lakini ni mwenye hekima , busara na msikivu.
Basi Rais akaniambia Said nimekuita Ikulu kwa ajili ya kuzungumza na wewe.Akaendelea kuniambia anataka tuzungumze kama Mama na Mtoto, aliamua kuweka urais pembeni ili tuwe huru.
Aliniambia nimekuita unieleze ya huko mtaani, akaniambia najua unakaa Majohe kwa Ngozoma, nikamwambia ni kweli Mheshimiwa Rais.
Akaniambia tena najua Wilaya yako ni Kilosa mkoani Morogoro nikamjibu tena ndio , huku nikiinamisha kichwa chini kuonesha ishara ya utiifu kwake.Akaniuliza nilienda Kilosa lini, nikimajibu mwanzoni mwa mwaka huu, akaniuliza Kilosa wanasemaje nikamjibu wako salama ila changamoto ni wakulima na wafugaji bado kuna muingiliano wa maeneo ya malisho na kulima.
Lakini nikampongeza Rais kuhusu hatua anazochukua kwani hali ilivyo sasa ni tofauti na hapo miaka ya nyuma,kuna unafuu kidogo ingawa wakulima wanalalamika mifugo kuharibu mazao yao, mazao yanaliwa na ng'ombe.Katika hilo akanijibu anafahamu lakini kwa sasa hali inaridhisha, migogoro imepungua.
Akaendelea kusema viongozi wa Mkoa wa Morogoro wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Adam Malima wako imara lakini Kilosa yuko Shaka Hamdu Shaka anafanya kazi nzuri.Wakati huo nilikuwa namsikiliza na mwisho nikamwambia ahsante Rais wangu kwa hatua unazochukua kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji katika maeneo mbalimbali nchini kwetu.
Lakini akaniuliza mtaani wanasemaje kuhusu mkakati wa kuendeleza bandari ha Dar es Salaam, nikamuangalia Rais kwa tabasamu na kumwambia hakika wengi wamefurahishwa na hatua unazochukua kuendeleza bandari ya Dar es Salaam pamoja na bandari zote nchini, fedha unazoweka kuboresha miundombinu Watanzania ni mashahidi.
Hata hivyo nikajikita katika bandari ya Dar es Salaam nikaendelea kumwambia mwanzoni wapo waliokuwa wanapinga uwekezaji unaotaka kufanywa na DP World katika bandari ya Dar lakini shida ni elimu na sasa wengi wanaelewa dhamira yako njema mheshimiwa Rais.
Na baada ya kusikia tayari mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na DP World umesainiwa wamefurahi na wanakupongeza sana.Wanaimani kubwa na wewe na katika hili wanakuunga mkono.
Rais wakati namueleza alikuwa kimya ananisikiliza na nilipomaliza kuzungumza akaniambia anafahamu yote yaliyokuwa yanazungumzwa na yote ameyazingatia huku akisisitiza lengo kubwa ni kuboresha uendeshaji wa huduma katika bandari hiyo ili kwenda sambamba na ushindani uliopo.
Hata hivyo Rais Samia hakuishia hapo akaniuliza tena vipi huko mtaani wanasemaje kuhusu uongozi wangu, aliponiuliza hivyo sikutaka kuchelewa wala kujifikiria, nilimjibu mimi pamoja na Watanzania wote tunaridhishwa na uongozi wako.
Nchi yetu iko salama, tuna utulivu na kila mtu anaendelea na shughuli za ujenzi wa taifa. Nikamwambia Rais Samia uongozi wako umeleta faraja katika mioyo ya watu wengi, umeponesha majeraha yaliyopo moyoni, umerejesha utulivu maeneo ya kazi.
Rais uongozi wako umeendelea kutupa kipaumbele wananchi wote na kubwa zaidi uamuzi wako wa kutoa fedha kusomesha watoto wa taifa hili kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha sita hakika umetuondolea mzigo mkubwa.
Wakati huo Rais ananisikiliza kwa umakini mkubwa, lakini akauliza kama kuna changamoto nyinyine ambazo zinalalamikiwa katika eneo la elimu, kimsingi nilimwambia hakuna ingawa michango mashuleni imerudi na wazazi na walezi wanaanza kulalamika.Hapo Rais akajibu kwa kifupi tu kwamba atachukua hatua.
Lakini katika mazungumzo yetu Rais aliniuliza ninaonaje eneo la sekta ya afya, nikamjibu kwa kifupi tu, tunashukuru kwa hatua ambazo serikali inaendelea kuchukua, tumeona Bohari ya Dawa inavyoimarisha utoaji huduma , dawa na vifaa tiba angalau malalamiko yamepungua, lakini tunashuhudia ujenzi wa miundombinu wa vituo vya afya, zahanati, hospitali za rufaa.
Hata hivyo nilimuomba Bima ya Afya kwa Wote mchakato uende kwa haraka, gharama za matibabu ziko juu, tukiwa na bima ya afya kwa wote itatupa uhakika wa matibabu.Rais alijibu mchakato unaenda vizuri na utakamilika kwani dhamira ya Serikali yake ni kuhakikisha watanzania wanakuwa na bima ya afya.
Hakika mazungumzo yangu na Rais yalikuwa mazuri.Aliniuliza kama kuna chochote nataka kuomba msaada wake, lakini kabla ya kujibu ikanijia barabara yetu ya Majohe kwa Ngozoma hivyo nikamwambia ninachotamani unisaidie basi kwa niaba ya wakazi wa Majohe kwa Ngozoma tunaomba barabara ya lami.
Akacheka na kisha akajibu hilo atazungumza na Waziri wa Ujenzi.Nikamwambia Rais ahsante na natanguliza shukrani kwako kwa niaba ya wananchi .
Hata hivyo tukazungumza kuhusu Chama chake cha CCM, aliniuliza naonaje mwenendo wa Chama hicho, nilimjibu kwa kujiamini kwamba Rais najua wewe ndio Mwenyekiti wa CCM Taifa hivyo unakijua vizuri kuliko mimi...
Lakini kwa kuwa umetaka maoni yangu nakupongeza kwa jinsi unavyokisimamia Chama, umeteua watu sahihi kuanzia Makamu Mwenyekiti wako Abdulurhaman Kinana, Katibu Mkuu Daniel Chongolo lakini pamoja na sekretarieti yako iko vizuri.Rais akaniangalia lakini hakunijibu kitu zaidi ya kuonesha ishara ya kichwa kwamba anakubali nilichokisema.
Kabla hajasema chochote nikampongeza Rais Samia pia kwa uamuzi wake wa kumteua Jokate Mwegelo kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania(UWT) nikamwambia Jokate ni mtu sahihi na kubwa zaidi ni mbunifu.Rais akatabasamu , hakusema chochote.
Wakati tunaendelea na mazungumzo aliniuliza kuhusu michezo na jitihada zinazofanywa na Serikali yake hapo nikamwambia Rais mtaani wananchi hasa wadau wa michezo wanakupongeza.
Wanaona juhudi zako binafsi ikiwemo ya kutoa motisha kwa timu zinazoshiriki michuano ya kimataifa kwa kutoa fedha kwa kila goli, lakini tunaona uboreshaji wa viwanja vya michezo.Katika michezo Rais unaupiga mwingi sana .
Nilivyosema Rais anaupiga mwingi akacheka na kisha akasema hayo maneno ya kuupiga mwingi tunaacha kwenu, sisi Serikali lengo letu ni kuona michezo yote inapewa nafasi katika jamii.
Hata hivyo nilimuuliza yeye ni shabiki wa timu gani kati ya Simba na Yanga, hapo hakujibu chochote .Nikamuuliza tena swali hilo hilo hakujibu, lakini wakati huo akawa anasimama.Nikaona anakuja nilipokaa,akaniomba nisimame.
Na kisha akaniambia kwa sauti ya chini kwamba ameniita ili kunipa mtaji wa kufanyabiashara nayotaka, akatoa bahasha ya kaki na kuniambia ameniwekea Sh.milioni 10, nakashtuka kwa mshangao, kweli mimi wa kupewa hela na Rais, basi nikamwambia Rais wangu ahsante ahsante ahsante.
Ahsante sana Mama kwa upendo wako.Ahsante kwa kunipa zawadi hii ya mtaji.Lakini wakati naendelea kumshukuru Rais wangu kwa kunipa mtaji nikaona ananipa na hati ya kiwanja na kiwanja chenyewe kipo Chamwino Dodoma.Nikapokea lakini nilishindwa kuvumilia nikamuuliza kwanini Mheshimiwa Rais umenipa vyote hivi.
Rais wakati anataka kuanza kujibu nikashutuka na nikawa nawaza niko wapi, kumbe nilikuwa ndotoni tu.Kumbe sikuwa Ikulu bali niko kitandani huku uswahili kwetu.Narudia tena kumbe sikuwa Ikulu, wala sikuitwa na Rais na hakuna chochote tulichozungumza naye.
Ni ndoto niliyoota tena mchana wa jua kali baada ya kushiba ugali na maharage, mpishi mama Faisal.Uliyesoma hapa narudia tena ilikuwa ni ndoto na nashangaa kuota ndoto ya namna hii.Sijui imekuaje aiseee.Alamsiki
0 Comments