Ticker

6/recent/ticker-posts

TRA YAFAFANUA MADAI YA MFANYABIASHARA EMMANUEL GADI

Na: Mwandishi Wetu


12 Oktoba, 2023

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) haina mfumo wowote mwingine inaouendesha wa kuingiza mizigo nchini nje ya mfumo wa Forodha wa TANCIS ambao unatumika kwa mujibu wa Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA Bw. Stephen Kauzeni kwa waandishi wa habari wakati akitoa ufafanuzi juu ya taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu malalamiko ya Bw. Emmanuel Gadi ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Wintech Tanzania Ltd anayedai kuwa, TRA imetengeneza mfumo wa kuingiza mizigo nchini nje ya mfumo halali wa Serikali kinyume na Sheria ya Forodha.

“Bw. Emmanuel Gadi alifikisha malalamiko yake kwa njia ya barua tarehe 27 Februari, 2023 akidai kupewa uthibitisho na TRA wa kuingiza mzigo wa vifurushi 471 vya Toner Cartridges kupitia kampuni ya Tosh Logistics Ltd.

TRA ilifanya Uchunguzi wa kutosha na kuthibitisha kwamba hapakuwa na mzigo wowote ulioingizwa nchini kwa jina la Wintech Tanzania Ltd wa vifurushi 471 vya Toner Cartridges kupitia kadhia yenye namba TZDL – 22-1382193 ya tarehe 18 Agosti 2022 kama anavyodai,” amesema Bw. Kauzeni.

Ameongeza kuwa, TRA ilimjibu mhusika kupitia barua yenye kumbukumbu namba CF 8/92/01 ya tarehe 25 Julai 2023 ikimjulisha kuwa, kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa House Bill of Lading na kutoonekana kwa mzigo huo kwenye kadhia iliyowasilishwa na kampuni ya Tosh Logistics Ltd, TRA isingeweza kuthibitisha kuingizwa kwa mzigo huo nchini.

“Kupitia taarifa ya Bw. Emmanuel Gadi aliyoitoa kwenye vyombo vya habari, tumebaini kuwepo kwa viashiria vya ukwepaji kodi kwani ni dhahiri kuwa mzigo wake uliingizwa kwa njia za magendo,” ameeleza Meneja Kauzeni.

Meneja huyo wa Elimu kwa Mlipakodi amemtaka mlalamikaji kuwasilisha nyaraka na uthibitisho wa Kampuni yake kuingiza mzigo huo nchini mara moja ili hatua stahiki zichukuliwe.
Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Stephen Kauzeni akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati akitoa ufafanuzi juu ya taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu malalamiko ya Bw. Emmanuel Gadi ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Wintech Tanzania Ltd anayedai kuwa, TRA imetengeneza mfumo wa kuingiza mizigo nchini nje ya mfumo halali wa Serikali kinyume na Sheria ya Forodha (Picha na Mpiga picha wetu).

Post a Comment

0 Comments