Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUMBO AFANYA MAZUNGUMZO NA WAZIRI WA MIFUNGO NA UVUVI

Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega katika kikao kilicholenga kufahamu vipaumbele muhimu vya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambavyo vitajumuishwa katika mapendekezo yatakayosaidia kuandaliwa kwa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2024/2025.

Kikao hicho kimefanyika Oktoba 23, 2023 katika Ofisi za Wizara ya Mifugo na Uvuvi, jijini Dodoma.

Prof. Kitila amesema kikao hicho pia kimelenga kuleta ushirikishwaji wa sekta katika maandalizi ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2024/2025

Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega ameahidi kufanya kazi kwa karibu na Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji ili sekta za mifugo na uvuvi ziweze kutekeleza majukumu yake sambamba na Mpango wa Maendeleo wa Taifa.

Aidha, Mhe. Ulega ameomba masuala yanayohusu uanzishwaji wa Mamlaka inayosimamia Uvuvi, Chanjo ya Mifugo , Bandari ya Uvuvi ya Bagamoyo na Uchumi wa bluu na Programu ya Jenga Kesho Iliyobora (BBT-LIFE) kujumuishwa katika mpango wa maendeleo wa mwaka 2024/2025.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida ametoa rai kwa Wizara hiyo kuzingatia uzalishaji wenye tija na upatikanaji wa masoko wa bidhaa zinazozalishwa huku akigusia matumizi ya teknolojia katika uzalishaji akitolea mfano ufugaji wa Samaki.

Naye, Katibu Mtendaji, Tume ya Mipango Bw. Lawrence Mafuru amesisitiza kila sekta kufikiria Sekta nyingine ambayo inaweza kushirikiana nayo kipindi inapanga Mipango yake.

Pia, amesisitiza kuangalia namna vipaumbele vinavyotolewa vinaweza kuchangia ukuaji wa Sekta na Uchumi wa Taifa.

Post a Comment

0 Comments