TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) inatarajia kutoa sh mil 450, kwa watafiti watano watakaochaguliwa na wataalamu wa ubiasharashiji na utafiti katika kinyang'anyiro cha ushindani.
Hayo yalisemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uendelezaji na Uhawilishaji wa Teknolojia (CDTT) COSTECH Dkt. Gerald Kafuku wakati akifungua mashindano ya tafiti hizo yaliofanyika tarehe 20 Novemba, 2023 Kibaha, mkoani Pwani.
Tafiti zitakazochaguliwa zitapelekwa sokoni kwaajili ya ubiasharishaji na kutatua changamoto zinazokabili jamii.
Dkt. Kafuku amesema maombi ya ubiasharishaji wa matokeo ya Ubunifu hayo yalipatikana mara baada ya COSTECH kutoa tangazo la ndani kwa Vyuo Vikuu ambavyo viko kwenye Mradi wa mageuzi ya kiuchumi katika Elimu ya Juu (HEET).
Amesema wamefanya hivyo ili Vyuo waweze kuomba na Vyuo viliitikia wito huo ambapo jumla ya tafiti 66 ziliomba na mchujo ukafanyika mpaka kufikia tafiti 22 na baadaye zikabaki 6, kati ya hizo tunatarajia kupata 5 kama zitakazofuzu katika usahili huo.
Dkt. Kafuku amefafanua kuwa baada ya kupokea machapisho hayo walifanya Mafunzo ya siku tatu jinsi ya kuandika miradi yenye tija katika uchumi na jamii na walipata muda kuboresha maandiko yao na kuweza kuingia kwenye hatua nyingine za uchujaji.
Amesema hii itakuwa chachu kwa Vyuo Vikuu kutenga fedha ili kugharamia matokeo ya Utafiti kwenda katika Jamii.
Kwa upande wake Dkt. Erasto Mlyuka ambaye ni Meneja wa Usimamizi na Uhawilishaji wa Teknolojia COSTECH na msimamizi wa programu ya kuendeleza tafiti kwenye ubiasharishaji, amesema wanataka tafiti zinazopatikana katika Taasisi za Elimu ya Juu ziweze kuwa na manufaa makubwa kwa jamii.
Dkt. Mlyuka amesema namna gani hizi tafiti zitatoka katika makabati ni kwa kupitia hatua mbili yaani kupitia Vyuo Vikuu vinavyoshiriki katika Mradi wa HEET kuona kama wana Sera ya miliki dhihini (Institutional IP policy) huo ndio unakuwa msingi wa kuratibu namna ubiasharishaji wa tafiti na bunifu zao unavyoweza kufanyika.
0 Comments