Ticker

6/recent/ticker-posts

HAKUNA HAKI BILA WAJIBU-DKT ANDILILE


Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa EWURA wakati wa kikao cha kwanza cha mkutano wa pili wa Baraza, uliofanyika tar 8-9 Novemba 2023 jijini Dodoma.


Katibu Mkuu TUGHE Taifa, Ndugu Rugemalira Rutatina akizungumza wakati wa Kikao cha Kwanza cha Mkutano wa pili wa Baraza la Wafanyakazi wa EWURA, kilichofanyika 8-9 Novemba, 2023 jijini Dodoma.



Baadhi ya Washiriki wa Kikao cha Kwanza cha Mkutano wa Pili wa Baraza la Wafanyakazi wa EWURA wakifuatilia mada kuhusu tathmini ya utendaji wa EWURA kwa mwaka wa fedha 2022/23 wakati wa kikao hicho.

Na.Mwandishi Wetu_DODOMA

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Dkt. James Andilile, amewataka wafanyakazi wa Mamlaka hiyo kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo ili kuleta tija na ufanisi katika majukumu yao ya kila siku.

Dkt. Andilile ameyasema hayo, leo 9/11/23 wakati akiahirisha kikao cha kwanza cha mkutano wa pilli wa Baraza la Wafanyakazi wa EWURA, kilichofanyika jijini Dodoma kwa siku mbili kuanzia 8 Novemba 2023.

“ Niwakumbushe wafanyakazi wenzangu, tudai haki zetu lakini tusisahau kuwa pia tunao wajibu juu ya haki hizo, ninawasisitiza kulizingatia suala hilo kwani sote tunafahamu hakuna haki bila wajibu”. Alisema Dkt Andilile.

Mkurugenzi Mkuu huyo, pia, amewasisitiza wafanyakazi kuwahi kazini, kuwa wamoja na kujiepusha na vitendo vya rushwa na kutekeleza majukumu waliyopangiwa kwa ufasaha bila kusukumwa, na kuwa kwa kufanya hivyo ni kuchochea uimara wa taasisi.

“Kwenye suala la rushwa, naomba niwe wazi, sitalivumilia, tutalifanyia kazi, haiwezekani viongozi watueleze suala hili mara kwa mara, wao wana taarifa nyingi, tujiangalie, lisemwalo lipo kama halipo laja” Alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Dkt. Andille amewaelekeza Wakuu wa Idara, Vitengo na Kanda kuwasimamia wafanyakazi katika maeneo yao ili kuhakikisha kuwa kila mmoja anatekeleza majukumu aliyopangiwa kwa wakati na kwa ufanisi.

“ Ninyi viongozi wenzangu, kwanza tuwe na utu, pili, waelimisheni walio chini yenu kuthamini kazi walizopewa, simamieni nidhamu, na sisi viongozi tuwe mfano, tukumbuke tumepewa dhamana kubwa” Alisema.

Naye Katibu Mkuu wa TUGHE ngazi ya Taifa, Bw. Rugemalira Rutatina ameeleza kwamba TUGHE itaendelea kutoa ushirikiano kwa tawi la EWURA katika kufanikisha majukumu yake.

“Niseme tu tutaendelea kuwasimamia, kuwaelimisha wajumbe wa Baraza kutambua wajibu wao na kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa tawi lenu, mnafanya vizuri” Alieleza

Katibu wa Baraza, Bw. Baraka Butoto aliwashukuru wajumbe wote kwa ushirikiano uliowezesha kufanikisha kikao hicho.

Post a Comment

0 Comments