Na WyEST, Dar es Salaam
Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) unaosimamiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia umeanzisha ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu ya Juu, Sekta Binafsi na Viwanda ili kusaidia upatikanaji wa wahitimu wenye ubora na wenye kuhitajika katika soko la ajira.
Akizungumza katika Mkutano wa wa Wakuu wa Taasisi za Elimu ya Juu na waratibu wa mradi huo kutoka katika taasisi hizo Novemba 13, 2023 Jijini Dar es Salaam Mratibu wa Mradi huo Dkt. Kenneth Hosea amesema Mradi wa HEET umewezesha kuanzisha kamati za ushauri zinazounganisha Vyuo Sekta Binafsi na viwanda zinazoshauri katika uandaaji wa mitaala ambayo itakuwa na tija.
Dkt. Hosea amesisitiza kuwa ni vema kwa watu wa sekta binafsi na viwanda kusaidia upatikanaji wa wahitimu wenye ubora kwa kushiriki katika kutoa maoni katika uhuishaji wa mitaala kwani wao ndio wenye uhitaji na wanajua wanachohitaji kutoka kwa wahitimu pamoja na kuongeza udahili vyuoni na kutengeneza wahitimu wenye ubora katika kazi na ujuzi.
“Wizara za ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia mradi wa HEET ina matumaini kuwa Sekta binafsi na viwanda vitasaidia katika kuhuhisha mitaala yetu nchini pamoja na ushirikiano huu usaidia na kujenga uelewa juu ya kazi za kamati na kusaidia vyuo vyetu kuzalisha watu wenye ujuzi” amesema Mratibu huyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Masuala ya Ushirikiano wa Viwanda na Taasisi za Elimu ya Juu Dkt. Hadija Kweka amesema kamati hizo ambazo zimeanza kufanya kazi zimekuwa na faida kubwa katika kusaidia Taasisi za elimu ya Juu kufahamu ni aina gani ya mafunzo yanayopaswa kutolewa kwa ajili ya mahitaji ya soko la ajira.
Dkt Kweka amesema Mkutano huo unalenga katika kuhakikisha ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu ya Juu, Sekta Binafsi na Viwanda unawasaidia wanafunzi wa elimu ya juu kupata ujuzi ambao haupatikani katika vyuo lakini wanaweza kupata wanapokuwa katika mafunzo kwa vitendo katika viwanda na makampuni mbalimbali, hivyo mkutano huo unajadili kwa pamoja namna ya kuwasaidia kupata nafasi za kufanya mafunzo kwa vitendo kwa kusimamiwa kwa ukaribu.
Naye mmoja wa washiriki wa mkutano huo kutoka Kampuni ya Alfa Associate Limited Dkt. Alphonce Masaga amesema mkutano huo unalenga kuja na suluhisho la kuhakikisha wanafunzi wanaomaliza elimu ya juu wanaajiriwa kwa kuwawezesha kupata uzoefu wa kuwasaidia kuajiriwa
0 Comments