Ticker

6/recent/ticker-posts

NAIBU UMMY AZINDUA KLINIKI YA METHADONE NA JUMUIYA YA KIMATAIFA YA WATAALAM WANAOHUSIKA NA MASUALA YA KINGA NA TIBA KWA WARAIBU WA DAWA ZA KULEVYA NCHINI

NA. MWANDISHI WETU

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga leo tarehe 27 Novemba, 2023 amemuwakilisha Mheshimiwa Jenista J. Mhagama kuzindua kituo cha kutolea dawa ya Methadone (MAT Clinic) kwa waraibu wa dawa za kulevya aina ya heroine.

Akizindua kituo hicho kilichoko katika Gereza la Kihonda mkoani Morogoro Naibu Waziri Ummy amesema, uzinduzi wa kituo hicho unashabihiana na Dira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoelekeza kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya ikiwemo uimarishaji wa utoaji eilimu kinga, pamoja na upanuzi wa tiba na huduma za utengamao kwa waraibu wa dawa za kulevya nchini.

Aidha, ameishukuru Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Jeshi la Magereza kwa kukubali kituo hiki kujengwa katika eneo la Gereza la Kihonda, Wizara ya Afya kwa ushirikiano walioutoa wakati wa maandalizi ya ujenzi wa Kituo hiki, pamoja na wadau wengine wa maendeleleo ambao wamekuwa mstari wa mbele katika ujenzi/ukarabati na uendeshaji wa vituo vingine vya MAT vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini.

“Kipekee niushukuru Mfuko wa Dunia (Global Fund) kwa kukubali kufadhili ujenzi wa kituo hiki kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya. Kituo hiki kitaokoa maisha ya vijana wetu wengi wenye changamoto ya matumizi ya dawa za kulevya kwani kupitia kituo hiki huduma mbalimbali zitatolewa zikiwemo tiba ya uraibu kwa kutumia methadone, upimaji na matibabu ya UKIMWI, Kifua Kikuu, Magonjwa ya Akili, Homa ya Ini pamoja na magonjwa mengine yanayoambatana na uraibu wa dawa za kulevya” amesema Mhe. Ummy.

Akizungumzia uzinduzi wa Jumuiya ya Wataalam wanaohusika na Masuala ya Kinga na Tiba kwa waraibu wa Dawa za Kulevya, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema, Mamlaka imeona umuhimu wa kuanzisha Umoja huu (International Society for Substance Use Professionals – ISSUP Tanzania) ili kuimarisha na kuboresha utaalam katika masuala ya utoaji elimu sahihi, tiba na huduma za kijamii kwa waraibu wa dawa za kulevya kulingana na viwango vya kimataifa.

“Nakuomba Mheshimiwa Waziri uzindue Umoja huu kwa kuwa utaimarisha mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya pamoja na kupunguza tatizo la magonjwa ya UKIMWI, Kifua Kikuu, Magonjwa ya Akili, Homa ya Ini pamoja na magonjwa mengine yanayoambatana na uraibu wa dawa za kulevya” amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Ameongeza kuwa matukio haya mawili yanashabihiana na majukumu na mikakati ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwani yanaimarisha na kupanua huduma za tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya pamoja na upatikanaji wa elimu sahihi kuhusu madhara ya dawa hizo.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP) Mzee Ramadhan Nyamka,ameishukuru Mamlaka kwa kuwapa kazi ya ujenzi wa kituo hicho na kutoa rai kwa Taasisi nyingine za serikali kulitumia Jeshi la Magereza katika miradi ya ujenzi. Ameongeza kuwa kituo cha MAT kilichozinduliwa kitatumiwa na wafungwa na mahabusu wote nchini.

“Tatizo hili ni kubwa, na bila kuwasaidia kupitia tiba hii haiwezekani kufanikiwa katika programu ya urekebishaji. Wakishapona programu za urekebu zitakwenda vizuri” amesema CGP Nyamka.

Pamoja na hayo ametoa wito kwa wazazi kuwa karibu na watoto na kuwafuatilia nyendo zao ili tuwahi kuzuia tatizo la dawa za kulevya katika ngazi ya familia na kuendelea kuwa ka kizazi chenya afya bora na kujiletea maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

AWALI

Uzinduzi wa Kituo hiki cha kutolea tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya ni mwendelezo wa vituo vilivyojengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Dunia (Global Fund) hapa nchini ambapo mpaka sasa vimetimia vituo 16. Vituo vingine ni Kituo cha Tanga kilichopo katika Hospitali ya Mkoa ya Bombo kilichogharimu Zaidi ya shilingi milioni 900, Kituo cha Arusha kilichopo katika hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kilicho gharimu Zaidi ya Shilingi milioni 400, Ukarabati wa kituo cha Dodoma 5 kilichopo eneo la Itega na ukarabati wa vituo vidogo vine vilivyopo mkoani Dar es Salaamu ambapo kimojawapo kiko katika gereza la Segerea.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga akivuta kitambaa kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ufunguzi wa Kliniki ya Methodone katika Gereza la Kihonda pamoja na uzinduzi wa Jumuiya wa Kimataifa ya Wataalam wa Masuala ya kinga na tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya (ISSUP).Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini (DCEA), Kamishna Jenerali Aretas Lyimo na kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Rebeca Nsemwa na Mkuu wa Gereza la Kihonda SP Lucas Ambrose, tarehe 27 Novemba, 2027.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Kliniki ya Methodone katika Gereza la Kihonda pamoja na uzinduzi wa Jumuiya wa Kimataifa ya Wataalam wa Masuala ya kinga na tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya (ISSUP), kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Rebeca Nsemwa na kulia kwake ni Kamishna Jenerali Aretas Lyimo wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA)
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga akihutubia wakati wa hafla ya ufunguzi wa Kliniki ya Methodone katika Gereza la Kihonda pamoja na uzinduzi wa Jumuiya wa Kimataifa ya Wataalam wa Masuala ya kinga na tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya (ISSUP) kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama, hafla ilifanyika Mkoani Morogoro tarehe 27 Novemba, 2027.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Rebeca Nsemwa akitoa salamu za mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Adam Malima, wakati wa hafla hiyo.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Anderson Mutatembwa akizungumza wakati wa hafla ya Ufunguzi wa Kliniki ya Methodone katika Gereza la Kihonda pamoja na uzinduzi wa Jumuiya wa Kimataifa ya Wataalam wa Masuala ya kinga na tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya (ISSUP).
Baadhi ya washiriki hafla ya ufunguzi wa Kliniki ya Methodone katika Gereza la Kihonda pamoja na uzinduzi wa Jumuiya wa Kimataifa ya Wataalam wa Masuala ya kinga na tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya (ISSUP) wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi (hayupo pichani).
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga (kulia) akipanda mti mara baada ya ufunguzi wa Kliniki ya Methodone katika Gereza la Kihonda pamoja na uzinduzi wa Jumuiya wa Kimataifa ya Wataalam wa Masuala ya kinga na tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya (ISSUP), kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Rebeca Nsemwa.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Maafisa na Askari wa Gereza la Kihonda mara baada ya ufunguzi rasmi ya Kliniki ya Methodone katika Gereza hilo pamoja na uzinduzi wa Jumuiya wa Kimataifa ya Wataalam wa Masuala ya kinga na tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya (ISSUP) katika Gereza ya Kihonda Morogoro. 
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Ummy Nderiananga akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Rebeca Nsemwa mara baada ya kuwasili katika hafla ya ufunguzi wa Kliniki ya matibabu kwa waraibu wa Dawa za Kulevya katika Gereza la Kihonda pamoja na uzinduzi wa Jumuiya wa Kimataifa ya Wataalam wa Masuala ya kinga na tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya (ISSUP) katika Gereza ya Kihonda Morogoro. 

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

Post a Comment

0 Comments