Ticker

6/recent/ticker-posts

OPERESHENI MAALUM YA DCEA YABAINI KIWANDA CHA KUTENGENEZA BISKUTI ZENYE BANGI JIJINI DAR

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imekamata kilogramu 423.54 za bangi iliyosindikwa maarufu kama skanka katika operesheni maalum zilizofanyika kwenye mipaka na fukwe za Bahari ya Hindi.

Kilogramu 158.54 zilikamatwa eneo la Kigamboni na Kawe jijini Dar es salaam zikiwa zimehifadhiwa ndani ya mabegi ya nguo tayari kwa kusafirishwa, kilogramu 265.64 zilikamatwa katika matukio tofauti mikoa ya nyanda za juu kusini zikiwa zimefichwa ndani ya magari kwa kuchanganywa na bidhaa nyingine ikiwemo maboksi yenye matunda aina ya apples zikisafirishwa kuelekea jijini Dar es salaam.

Aidha, Mamlaka imekamata watu wanaojihusisha na utengenezaji wa biskuti kwa kuchanganya na skanka katika eneo la Kawe jijini Dar es salaam. Katika tukio hilo, watuhumiwa walikutwa wakiendelea na uzalishaji wa biskuti hizo kwa kutumia mtambo mdogo wa kusaga skanka na vifaa vya kutengeneza biskuti za bangi. Vilevile, Mamlaka imebaini maeneo yanayotumika kama masoko ya kusambazia na kuuza skanka kwenye fukwe za Bahari ya Hindi.

Kutokana na operesheni hizo, watu 16 wamekamatwa ambapo kati yao sita (6) wamefikishwa mahakamani na 10 watafikishwa baada ya taratibu za kisheria kukamilika.

Skanka (skunk) ni jina la mtaani linaloitambulisha aina ya bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu (TetraHydroCannabinol - THC) ikilinganishwa na bangi ya kawaida. Dawa hii ya kulevya hutokana na kilimo cha bangi mseto ambapo asilimia 75 ni bangi aina ya sativa na asilimia 25 ni bangi aina ya indica. Kiwango cha sumu kilichopo kwenye skanka ni zaidi ya asilimia 45 ukilinganisha na bangi ya kawaida ambayo kiwango chake cha sumu ni kati ya asilimia 3 mpaka 10. Hivyo, skanka ina madhara makubwa zaidi kwa mtumiaji ikiwemo kuamsha na kuzidisha magonjwa ya afya ya akili kwa haraka.

Imebainika kuwa, watu wasiowaaminifu huchanganya skanka kwenye vyakula kama vile biskuti, keki, jamu, sharubati, tomato sauce pia kwenye sigara na shisha. Lengo la kufanya hivyo ni kurahisisha uuzwaji wa dawa hizo kwa kificho na kuongeza idadi ya watumiaji wa dawa za kulevya hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya vyakula hivyo hupendwa na watoto.

Wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo wanapaswa kuwa makini na vyakula wanavyovitumia na kuacha kufuata mikumbo isiyofaa ikiwemo kutumia vilevi na vitu wasivyovijua hali ambayo inaweza kuwaingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya.

Aidha, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inaendelea kufanya operesheni dhidi ya wasafirishaji na wazalishaji wa dawa za kulevya katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha dawa za kulevya haziendelei kuwepo nchini.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inawaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za wahalifu wa dawa za kulevya kwa kupiga namba ya bure ya 119 ambapo taarifa zitapokelewa kwa usiri mkubwa na kufanyiwa kazi.

Post a Comment

0 Comments