Na Munir Shemweta, WANMM ARUSHA
Serikali imezitaka taasisi zilizopewa mamlaka ya upimaji kuhakikisha zinashirikiana na Wizara ya Ardhi pale zinapokwenda uwandani ili kusaidia kuondoa migogoro inayoweza kuanzishwa kutokana na kutojua uhalisia wa mipaka.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geofrey Pinda tarehe Novemba 23, 2023 jijini Arusha wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka pamoja na Kongamano la Taasisi ya Upimaji Tanzania (IST).
"Hapa mna wataalamu, wapima kutoka TAZARA, Mamlaka ya Reli na maeneo mbalimbali, mtumza ardhi mkuu ni Wizara ya Ardhi kwa hiyo tunatoa wito kwa taasisi hizo zinapokwenda uwandani zifanye mawasiliano na wizara ili kumbukumbu zinazokwenda kufanyika pale ziweze kuwa na uwiano.
Akitolea mfano wa mgogoro wa ardhi uliotokea mkoani Manyara, Mhe. Pinda amesema upo mgogoro ulisababishwa na upimaji uliovuka hadi eneo la hifadhi ambapo wakati wa kutafuta ufumbuzi ukawekwa mpaka wa kiserikali kutenganisha mkoa na kusababisha vijiji kugawanyika ambapo kijiji kimoja kilisomeka mikoa yote miwili jambo alilolieleza kuwa, ni dalili kwamba hakukuwa na mawasiliano mazuri.
Kwa kupitia mfano huo, Naibu Waziri wa Ardhi ametoa wito kwa taasisi yoyote inayopewa mamlaka ya upimaji kushirikiana na wizara ya ardhi ili kusaidia kuaondoa migogoro inayoweza kuanzishwa kutokana na kutojua uhalisia wa mipaka sambamba na kwenda bila wataalamu wa wizara na kusisitiza kuwa suala hilo lazima washirikiane kwa kuwa linaipelekea wizara changamoto nyingi.
Aidha, Mhe Pinda alitoa shukurani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa upendekeo kwa wizara ya ardhi hususan katika kuridhia miradi mikubwa ya maboresho ndani ya wizara.
Vile vile, aliwaambia washiriki wa mkutano huo kuwa wizara ya Ardhi imeanza kujenga mfumo wake wa TEHAMA wenye lengo la kufanya maboresho yatakayowezesha kuwa na ardhi kiganjani ili kuondoa changamoto za sasa kama vile uwepo viwanja pandikizi sambamba na kuwezesha wananchi kupokea taarifa pamoja na kuwasilisha malalamiko na maombi ya viwanja kupitia ardhi mtandao jambo alilolieleza litaondoa vishoka
"Nitoe wito na angalizo kwa taasisi na makampuni binafsi tuendako tunaenda katika ardhi mtandao muwe karibu na wizara ili kuwa sambamba na mabadiliko haya" alisema Pinda.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mansoor Hamdoun amesema, wizara ya Ardhi inaendeea na mikakati ya kuhakikisha inaboresha huduma zinazotolewa na wizara ikiwemo sehemu ya idara ya upimaji na ramani aliyoieleza kuwa ni idara kongwe katika wizara hiyo.
Ametanabahisha kuwa, ipo miradi mikubwa miwili ukiwepo wa ule wa milki salama za ardhi unaotokana na mkopo wa Benki ya Dunia aliouleza kuwa unatarajia kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya ardhi ikiwemo eneo la upimaji na ramani.
Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Taasi ya Wapima Tanzania (IST) unashirikisha wataalamu wa upimaji na ramani kutoka wizara ya ardhi, taasisi za umma pamoja na kampuni binafsi ambapo mbali na mambo mengine mkutano huo utatumika kufanya uchaguzi wa viongozi wa Taasisi hiyo.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geofrey Pinda akizungumza wakati wa kufungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Taasisi ya Wapima Tanzania (IST) jijini Arusha Novemba 23, 2023
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geofrey Pinda akizungumza wakati wa kufungua Mkutano Mkuu wa Mwaka Taasisi ya Wapima Tanzania (IST) jijini Arusha Novemba , 2023
Sehemu ya washiriki wa mkutano Mkuu wa Mwaka wa Taasisi ya Wapima Tanzania (IST) unaoendelea jijini Arusha.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geofrey Pinda akimkabidhi Cheti Makamu wa Rais wa Taasisi ya Wapima Tanzania (IST) Simon Chuwa wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Taasisi ya Wapima Tanzania (IST) jijini Arusha Novemba 23, 2023
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geofrey Pinda akiangalia kifaa cha upimaji alipokwenda kufungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Taasisi ya Wapima Tanzania (IST) jijini Arusha tarehe 23 Novemba 2023
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geofrey Pinda akiwa katika picha ya pamoja na wapima wanawake alipokwenda kufungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Taasisi ya Wapima Tanzania (IST) jijini Arusha tarehe 23 Novemba 2023.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geofrey Pinda akiwa katika picha ya pamoja na wapima waliohudhuria Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Taasisi ya Wapima Tanzania (IST) jijini Arusha tarehe Novemba 23, 2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
0 Comments