Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUMIMINA MAJI SINGIDA MASHARIKI.


SERIKALI imemuhakikishia Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu kuwa katika mwaka ujao wa fedha wa 2024/2025,watasambaza maji katika visima vyote vilivyochimbwa kwenye Jimbo hilo ili kuwaweza wananchi kupata majisafi na salama.

Aidha, imesema imeandaa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa kuanzia 2022/2023 hadi 2025/2026 wa kujenga mabwawa ya kuvuna maji ya mvua ili yatumike wakati wa kiangazi sambamba na kudhibiti mafuriko.

Mpango huo utasaidia kuhakikisha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira zinatosheleza katika Wilaya ya Ikungi Ikiwemo kata za Kikio, Misughaa, Lighwa, Mungaa, Siuyu, Issuna na Mkiwa.

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Marryprisca Mahundi amesema hay oleo Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu.

Katika swali lake Mbunge huyo ametaka kujua ni lini serikali itachimba Mabwawa ya maji Kata za Kikio, Misughaa, Lighwa, Mungaa, Siuyu, Issuna na Mkiwa ili kumaliza changamoto ya uhaba wa maji.

Akijibu swali hilo Marryprisca amesema katika mwaka 2024/2025 ,itafanya usanifu wa kina wa kubaini maeneo yanayofaa kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa katika kata hizo.

Amesema Wilaya ya Ikungi ina jumla ya Kata 28 zikiwemo kata za Kikio, Misughaa, Lighwa, Mungaa, Siuyu, Issuna na Mkiwa ambapo vyanzo vikuu vya maji katika Kata hizo ni maji chini ya ardhi kupitia visima vilivyochimbwa na kuwekewa miundombinu ya kutolea maji.

Aidha,amesema vijiji vyote vya Kata za Mungaa, Siuyu, Issuna na Mkiwa vinapata huduma ya maji kwa kutumia visima vilivyochimbwa kwenye vijiji hivyo.

Amefafanua kuwa baadhi ya vijiji katika Kata za Kikio, Misughaa na Lighwa bado havijapatiwa huduma ya maji ya kutosheleza.

Katika swali la nyongeza, Mbunge huyo ametaka kujua mpaka sasa upatikanaji wa maji katika wilaya ya Ikungi ni asilimia 53 ambayo iko chini sana na kuna maeneo ambayo yana changamoto kubwa .

“Mh Spika nataka nijue ni nini mpango wa serikali wa muda mfupi kuwapatia maji wananchi wa wilaya ya Ikungi kwa maana ya Kata za Kikiyo katika kijiji cha Nkundi, Isuna katika kijiji cha Isuna A kitongoji cha Manjaru,

“Pia nataka kujua ni lini serikali itatenga fedha kujenga miundombinu ya maji katika vijiji vya Msule , Munkinya , Mang’onyi, Mbwanjiki pamoja na Ujaire ili kuondoa adha ya maji katika maeneo niliyotaja,”amehoji Mtaturu.

Akijibu maswali hayo Marryprisca amesema mpango wa muda mfupi ni kwamba wataendelea kufanya jitihada za kuhakikisha visima vinachimbwa.

“Naomba nitumie Bunge lako Tukufu kumwagiza Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA),Mkoa wa Singida ahakikishe anakwenda kwenye hizi Kata wafanye usanifu ili kuona wapi tunaweza kupata maji chini ya ardhi ili waweze kupelekewa gari wachimbe visima na wananchi wapate huduma ya majisafi na salama,”amesema Marryprisca.

Aidha,amesema kwa utaratibu wa wizara visima vikishachimbwa kazi inayofuata ni usambazaji wa maji,“Nina uhakika kama mwaka huu wa fedha kwa maana ya kuanzia leo mpaka June wizara tukawa tumepata fedha ambazo hazitoshelezi kuwafikieni basi mwaka ujao wa fedha lazima maeneo haya yote tuje tusambaze maji katika visima ambavyo tumechimba,”amemuhakikishia Mtaturu.

Post a Comment

0 Comments