*Dkt.Jabir asema zama za sasa ni zama za taarifa
Na Chalila Kibuda
SERIKALI imetoa wito kwa wakuu wa shule za msingi na sekondari pamoja na vyuo wahamasishe kuanzisha klabu za kidijiti ili kufuata misingi na maadili na kuleta tija katika maendeleo ya Tehama nchini.
Wito huo umetolewa Jijini Dar es salaam katika uzinduzi wa kitabu Cha uwanzishaji na uratibu wa Klabu za kidijiti.
Akizungumza katika hafla ya Uzinduzi huo Katibu Mkuu Wizara ya habari mawasiliano na Teknolojia ya habari, Mohammed Khamis Abdulla alisema kuanzishwa kwa kitabu hicho ni muongozo wa vijana kupata fursa ya mapinduzi ya kidijiti.
"Kupitia kitabu hiki kitasaidia kuleta dira ya ubunifu katika nchi ambapo
Sera ya mwaka 2016 ipo kwenye mchakato wa kubadilishwa ambapo itachochea ntalanta na kuandaa sera ya kampuni changa ambayo itawasaidia wanafunzi kuwa wadau wakubwa, katika masuala hayo,"alisema
Alisema kujenga Taifa la kidijitali kupitia Klabu hizo zitachangia ufumbuzi na kuwawezesha vijana kuwa wabinifu na wajasiliamali.
"Wanafunzi wakijifunza TEHAMA wanakuwa Bora zàidi na kukuza uchumi na kusaidia mikakati ya kukuza taaluma hiyo,"alisema.
Hata hivyo alisema Wizara itaongoza safari hiyo ya kidijitali ili nchi ifike katika uchumi ya kidijitali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt Jabir Bakari alisema klabu za kidijiti ni majukwaa ya hiari yanayowakutanisha wanafunzi wa rika moja kupata uelewa na kuhamasishana juu ya tehama na kufanya ubunifu wa kutatua changamoto katika jamii.
"Kupitia klabu hizi za kidijiti tunajenga jamii yenye ufahamu wa teknolojia ya kidijiti na iliyo na taarifa na fursa zake "alisema Dk.Bakari .
Dk. Bakari alisema lengo la uwekezaji kwenye tehama ni kuboresha na kuongeza ufanisi katika utoaji huduma Kwa wananchi na kuongeza uwezo wa wananchi kushiriki kikamilifu katika uchumi kidijiti.
Aliongeza kuwa dunia ipo katika zama za taarifa zinazoenda sambamba na uchumi wa kidijiti kutoka katika safari za zama za Mawe, Chuma na Sasa ni zama za taarifa.
"Katika zama hizi ambazo zinajulikana kama zama za mapinduzi ya nne ya viwanda tehama ndiyo nyezo muhimu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla akizungumza wakati wa Uzinduzi wa Klabu za kidijiti katika Shule za Msingi, Sekondari na vyuo Vikuu katika uzinduzi uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla akipiga makofi akiwa na Watendaji wa TCRA, Mwenyekiti wa Bodi pamoja na wageni waalikwa mara baada ya kuzindua kitabu cha Kidijiti , jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla akipata maelezo kutoka kwa Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) Khamis Mohd Ndogo kuhusiana na Teknolojia ya Ufugaji Kuku kwa Kutumia Tehama namna ya kupata taarifa katika banda katika Maonesho ya Mabanda kuhusiana ubunifu wa Kidijiti katika hafla ya uzinduzi Kitabu cha Kidijiti uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya wanafunzi wakiimba wimbo wa Taifa katika hafla ya uzinduzi wa Kidijiti , jijini Dar es Salaam.
0 Comments