Balozi wa Tanzania nchini Algeria Mhe. Iman Njalikai amesema Chemba ya Biashara ya Algeria imedhamiria kununua kahawa na ufuta kutoka Tanzania sambamba na kuimarisha biashara baina ya Tanzania na Algeria.
Balozi Njalikai amesema hayo leo Novemba 29 2023 baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Chemba ya Biashara ya Algeria Kamel HAMENNI kwenye maonesho ya Kimataifa ya Kuchakata Taka na Kuziongezea Thamani (REVED) yanayoandaliwa na Chemba ya Biashara ya Algeria kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Utunzaji Taka, yaliyofanyika katika viwanja vya maonesho vya SAFEX, Algiers.
Amesema kuwa katika kufanikisha mipango hiyo wamekubaliana kusaidia kukamilisha mpango wa uundwaji wa Baraza la Biashara kati ya Chemba hiyo na Chemba ya Biashara ya Tanzania ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano yaliyosainiwa wakati wa Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Algeria Agosti 2023.
Katika hatua nyingine, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) lilitumia fursa ya maonesho hayo kuonesha namna Tanzania ilivyopiga hatua katika kudhibiti matumizi ya mifuko ya plastiki.
“NEMC kupitia imeweza kuvutia wawekezaji kutoka Algeria kuwekeza kwenye eneo la vifungashio rafiki kwa mazingira hii itasaidia kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini” Amesema Balozi Njalikai.
Kupitia maonesho hayo yaliyoanza tarehe Novemba 27, 2023 na kutarajiwa kufungwa tarehe Novemba 30, 2023, Balozi Njalikai alipata fursa ya kuona Teknolojia mbalimbali zinazotumika kuchakata na kuongeza thamani ya taka zinazozalishwa kwenye maeneo mbalimbali ya miji.
0 Comments