Na Jesse Chonde – OR, MU
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida amesema kuwa Serikali imechukua hatua muhimu katika kuhakikisha sekta binafsi inakua na kufikia malengo yake kwa kuweka miundombinu rahisi ya sera za uwekezaji na biashara.
Ameyasema hayo hivi karibuni akiwa nchini Uholanzi wakati akifunga Kongamano la Uwekezaji na Biashara kati ya Tanzania na nchi hiyo.
Dkt. Kida amesema kuwa falsafa ya Tanzania inazingatia sekta binafsi kuwa nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi kama ilivyoelezwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa, hivyo Serikali inafanya kazi kwa karibu na sekta binafsi kwa kuweka sera zinalenga kufikia lengo hilo.
“Tanzania ina dhamira kamilifu ya kuendeleza ushirikiano na Uholanzi, tunatarajia ushirikiano wetu utaendelea kukua, nina imani kwamba jukwaa hili limeibua njia za kuendeleza na kuimarisha ushirikiano huu.” Amesema Dkt. Kida.
Ameongeza kuwa Kongamano hilo lenye kauli mbiu “Ushirikiano wenye Usawa kwa Maendeleo Jumuishi na Endelevu," limetoa nafasi kwa nchi zote mbili kubadilishana fursa zilizopo, kuimarisha ushirikiano na kukuza biashara na uwekezaji.
Wakati huohuo, Dkt. Kida amebainisha kuwa kuanzia mwaka 1997 hadi sasa, jumla ya miradi 178 ya Uholanzi imesajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) katika sekta za kilimo, utalii, viwanda na huduma. Aidha, Wadachi wamechangia katika sekta ya fedha nchini hususani katika sekta ya benki.
Dkt. Kida amesititiza “Natumai Mkataba wa Makubaliano baina ya TIC na Baraza la Biashara la Uholanzi na Afrika (NABC) utachangia kuongeza kiwango na thamani ya uwekezaji na biashara kati ya nchi zetu”.
Aidha, amewakaribisha wawekezaji kutoka Uholanzi kuongeza uwekezaji Tanzania ambako kuna fursa ya kuyafikia masoko makubwa ya biashara kama soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Eneo la Huru la Biashara Bara la Afrika (AfCFTA).
Kongamano hilo limewakilishwa na ujumbe wa Serikali na sekta binafsi ambapo wamejadiliana kuhusu fursa za biashara na uwekezaji na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
0 Comments