Ikiwa imebaki siku moja kabla ya kuanza kwa mkutano wao wa mwaka utakaofanyika Novemba 09 hadi 11, 2023 Mjini Unguja, wajiolojia kutoka ndani na nje ya nchi wameanza kuingia Zanzibar na kutembelea maeneo mbalimbali kwa lengo la kutalii na kujifunza jiolojia ya eneo hilo.
Wajiolojia wameanza ziara leo tarehe 07 Novemba 2023 kwa kutembelea Kisiwa cha Changuu, Nakupenda Sandbank na Ngome Kongwe. Ziara itahitimishwa kesho tarehe Novemba 08, 2023 kwa kufanya ziara ya Safari Blue .
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wajiolojia wanaoshiriki ziara hiyo wamesema maeneo waliyotembelea na wanayoendelea kutembelea yamewapa kufurahia uwepo wao Zanzibar, kupumzika na kuongeza uelewa wao juu ya jiolojia ya Zanzibar.
Kwa upande wake, mratibu wa ziara hiyo Bw. Japhet Fungo ambaye pia ni Mkufunzi Msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema kuwa uongozi wa Jumuiya ya Wajiolojia Tanzania uliamua kuandaa ziara hiyo kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuhamasisha utalii endelevu ikiwa moja ya maeneo muhimu ya Dira ya Maendeleo ya Zanzibar mwaka 2050.
0 Comments