Ticker

6/recent/ticker-posts

UNESCO YAWEZESHA MAFUNZO YA WALIMU TARAJALI KUFUNDISHA STADI ZA MAISHA


Bagamoyo

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO, kwa kupitia programu yake ya O3 na O3 PLUS kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), imetoa mafunzo kwa wahadhiri na wakufunzi kutoka taasisi za Vyuo vikuu na Vyuo Vya Ualimu. Mafunzo yanalenga kutoa elimu ya ufundishaji wa stadi za maisha zinazozingatia afya ya uzazi, VVU/UKIMWI, kupinga ukatili wa kijinsia na kuhusiana kwa heshima kwa walimu tarajali (wanafunzi wa ualimu).

Mafunzo haya yametolewa mjini Bagamoyo kwa wahadhiri na wakufunzi takribani 50 kutoka vyuo vikuu 10 na vyuo vya ualimu 8 vya mikoa mbalimbali hapa Tanzania. Ikiwa huu ni muendelezo wa utoaji mafunzo ya elimu ya ufundishaji wa stadi za maisha zinazozingatia afya ya uzazi, VVU/UKIMWI, kuzuia ukatili wa kijinsia na kuhusiana kwa heshima ambayo yamekua yakitolewa kwa walimu waliopo kazini (in-service Teachers).

Mafunzo haya yatawawezesha wahadhiri na wakufunzi kuwafundisha walimu watarajiwa mbinu mbalimbali za ufundishaji mada zilizopo kwenye mitaala zinazohusu stadi za maisha, afya ya uzazi, VVU/UKIMWI, kuzuia ukatili wa kijinsia na kuhusiana kwa heshima kwa kutumia miongozo ya ufundishaji walimu iliyopo kwenye mfumo wa mafunzo wa masafa wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE Learning management system) .

“Ili mwalimu wa kesho awe bora na kuweza kutimiza jukumu lake la kusaidia watoto na vijana kufanikiwa kielimu bila vikwazo vya afya na ustawi, tunatakiwa tuanzie pale anapoandaliwa, ndio maana tumekuja na mpango wa kuwezesha pia mafunzo ya walimu tarajali” – Mathias Luhanya, Mratibu wa programu za Elimu kwa Afya na Ustawi, UNESCO.

UNESCO kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya afya, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na wadau wa elimu mbalimbali inaunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha mazingira salama ya kujifunzia kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari,ikiwemo kupata elimu sahihi ya makuzi na ya afya ya uzazi inayozingatia umri, mila na desturi, kuzuia ukatili wa kijinsia, elimu ya VVU/UKIMWI na Kuhusiana kwa Heshima.

Mafunzo haya ni sehemu ya mpango wa ushirikiano kati ya UNESCO, Taasisi ya Elimu Tanzania na Vyuo vinavyotoa mafunzo ya ualimu unaolenga kuboresha mazingira salama ya kujifunza na kufundishia shuleni, kupitia kuwajengea uwezo walimu (utoaji mafunzo) na kusambaza miongozo inayohusu utoaji wa elimu husika. Mpango huu unalenga kuwafikia walimu tarajali 12,000 ifikapo Juni 2027.

Post a Comment

0 Comments