Ticker

6/recent/ticker-posts

NCHIMBI AANZA KAZI KWA MAMBO MATATU, AKIPOKELEWA ZANZIBAR

*Atema cheche akionya makundi ya uchaguzi, asema ni mjinga tu hukoleza moto baada ya kupakua

*Aweka msimamo dhamira ya kulinda Mapinduzi, kudumisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa, akiwataja ACT

*Aweka msimamo CCM kuongeza uimara kusimamia Serikali zote mbili

* Mapokezi makubwa yamsubiria Dar Es Salaam, Januari 20, 2024.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amekemea na kuonya tabia ya baadhi ya wanaCCM wanaovunja taratibu za Chama kwa kuendekeza makundi baada ya uchaguzi, akisema haikubaliki na haitavumiliwa ndani ya CCM.

Amesema kuwa ni muhimu kiongozi anayeshinda awe mnyenyekevu kutumikia nafasi yake aliyochaguliwa na yule anayeshindwa anapaswa kuvumilia hadi mwaka mwingine, huku akisisitiza kwamba mambo yote mawili, kushinda na kushindwa katika uchaguzi, huenda sambamba na mipango ya Mungu.

Ndugu Dkt. Nchimbi amesema hayo wakati akiwahutubia wanachama wa CCM na wananchi wa Zanzibar, waliojitokeza kwa wingi wakati wa mapokezi ya kumpokea kiongozi huyo, yaliyofanyika leo Ijumaa, Januari Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar, iliyoko eneo la Kisiwandui, Unguja.

Aidha, Ndugu Dkt. Nchimbi amesisitiza kuwa Chama Cha Mapinduzi kimedhamiria kwa dhati kuyaenzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na kuhakikisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, inadumishwa ikiwa ni sehemu mojawapo ya kuwaenzi waasisi wa Mapinduzi hayo, ambao walikusudia kuhakikisha Wazanzibar wote wanakuwa wamoja katika kutafuta ustawi na maendeleo ya Zanzibar, bila kujali tofauti za kisiasa, kidini, rangi, kabila, wala hali zao za maisha.

“Wanaccm wote tunapokwenda kwenye uchaguzi tutaanza kumnong'ononeza mtu mmoja unataka kugombea anakwambia anakuunga mkono anakuwa wa kwanza, unamnong'oneza wa pili, wa tatu, wa nne wakati mwingine wanafika 20,30,40 wakishafika hapo wanaitwa kundi kwa hiyo unakuwa na kundi lako wewe na wenzako, hivyo hivyo na mwingine na mwingine hivyo. Tukimaliza uchaguzi makundi lazima yafe. Unapotaka kupika ndiyo unawasha moto, ukiipua unauzima moto wako. Ni mjinga peke yake anayekoleza moto wakati keshapakua.

“Kwa hiyo nawasihi wana CCM habari za uchaguzi lazima ziishe, walioshinda lazima wawe wanyenyekevu na walioshindwa lazima wajue kushindwa au kushinda kuko katika mapenzi ya Mwenyezi Mungu utashindwa leo, utashinda kesho. Mimi nimegombea nadhani mara 27 nimeshindwa mara sita na wala haikuwa shida. Ukiamua kuwa mwanasiasa kushindwa nayo raha, kwanza ukiwa mwana siasa hujawahi kushindwa wewe siyo mwanasiasa,” amesema Ndugu Dkt. Nchimbi.

Ndugu Nchimbi amewahakikishia wanaCCM na wananchi kwa ujumla kuwa katika kipindi ambacho atakuwa Katibu Mkuu wa CCM, chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CCM Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Chama kitaimarisha usimamizi wa Serikali zake zote mbili, ili kuhakikisha zinatimiza wajibu wa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 – 2025 na kuwatumikia Watanzania kwa uadilifu mkubwa.

“Kazi anayofanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar ni kubwa, inahitaji tu wana CCM kupitia chama chao kuimarisha usimamizi wa Serikali hizi. Ninawakikishieni tutazisimamia Serikali hizi, chini ya Mwenyekiti wetu wa Chama Cha Mapinduzi,” amesema Ndugu Nchimbi.

Kuhusu msimamo wa CCM ukudumisha dhamira ya waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar na kuimarisha umoja, utulivu na amani ya Wazanzibar, Katibu Mkuu Ndugu Nchimbi amesisitiza kuwa lazima wanaCCM waungane na wasikubali kuyumbishwa katika suala hilo, akitoa wito kwa Chama cha ACT Wazalendo, ambacho kiko katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, kuwa tayari kuzungumza linapotokea jambo lolote la kujadili.

“Mmenipeleka kwenye kaburi la muasisi Abeid Aman Karume na kila kiongozi anapokabidhiwa ofisi ya kitaifa anapokuja hapa Afisi Kuu kwa mara ya kwanza lazima apelekwe kufanya dua kwenye kaburi la mwasisi wetu na walioweka utaratibu huu hawakutaka tuishie kufanya dua pekee walimaanisha kutukumbusha kwamba Chama hiki ni cha kimapinduzi. Serikali yetu ni Serikali ya Kimapinduzi ni Serikali iliyopatikana kwa maamuzi ya ASP kutaka kuikomboa nchi yetu kuwarudishia walio wengi madaraka waongoze nchi yao wajitafutie maendeleo.

“Ukiona mtu ana hamu hamu hivi ya kuona Serikali ya Umoja huu imevunjika ujue muda wote anapotembea pua zake zinatamani damu za watu kwa hiyo lazima tuungane tushirikiane wana CCM wote msimamo wetu uwe mmoja tusiyumbishwe. Tunawapa shime wenzetu wa ACT-Wazalendo kwamba wajue nao wana wajibu wa kuunga mkono Serikali ya Umoja wa kitaifa na kama kuna mambo madogo madogo tuzungumze,” amesema Ndugu Nchimbi.

Akimkaribisha Katibu Mkuu Nchimbi kuzungumza, Naibu Katibu wa CCM Zanzibar, Ndugu Mohammed Said Mohammed (Dimwa), mbali ya kumpongeza Dkt. Nchimbi kwa kuteuliwa kutumikia dhamana hiyo, akimwelezea uwezo wake, alisema kuwa CCM ndiyo chama pekee chenye nguvu na uwezo wa kwamba nguvu hizo zinatokana na umoja wa wanachama, fikra sahihi za CCM na kukubalika kwake na umma hivyo kulinda na kuendeleza mambo hayo ni wajibu wa kwanza wa kila mwananchama.


Post a Comment

0 Comments