Ticker

6/recent/ticker-posts

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA MABORESHO YA KANUNI ZA MADALALI

Na Munir Shemweta, WANMM

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo imeipongeza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika Marekebisho ya Kanuni za Uteuzi, Malipo na Nidhamu kwa Madalali wa Baraza na Wasambaza Nyaraka za mwaka 2023 katika Sheria ya Mahakama za Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi Sura ya 216.

Akizungumza wakati wa wasilisho la Taarifa ya marekebisho hayo tarehe 19 Januari 2024 jijini Dodoma, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Ramadhani Suleiman Ramadhani amesema, wizara hiyo imezingatia mapendekezo ya Kamati katika kufanya maboresho na kamati yake haina budi kuipongeza Wizara ya Ardhi kwa kazi nzuri.

‘’Wizara imezingatia mapendekezo ya Kamati hivyo niwapongeze kwa kazi nzuri ya kufanya marekebisho yaliyozingatia maoni ya Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo ‘’ alisema Mhe. Ramadhani.

Mjumbe wa Kamati hiyo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu mkoani Mtwara Yahya Mhata amesema, maboresho yaliyofanyika yanonesha jinsi gani Wizara ya Ardhi ilivyo jipanga na kutoa pongeza kwa wizara hasa Katibu Mkuu wa wizara hiyo aliyemueleza kuwa ndiye Mtendaji Mkuu.

‘’Wizara iko ‘smart’ napenda niishukuru na kuipa pongezi kwa maboresho ya Kanuni za Madalali na zaidi nimpongeze Mtendaji Mkuu wa wizara’’ alisema Yahya.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sheria Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Method Msokele aliwaeleza wajumbe wa kamati kuwa, Kanuni zilizofanyiwa marekebisho zitajulikana kama Kanuni za Marekebisho ya Kanuni za Uteuzi, Malipo na Nidhamu kwa Madalali wa Baraza na Wasambaza Nyaraka za mwaka 2023.

‘’Kanuni hizi zitasomwa pamoja na Kanuni za Uteuzi, Malipo na Nidhamu kwa Madalali wa Baraza na Wasambaza Nyaraka za mwaka 2023 ambapo hapa zitarejewa kama Kanuni Kuu’’. Alisema Msokele.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda aliishukuru Kamati kwa ushauri wake wakati wa kufanya marekebisho ya kanuni za Madalali na kuahidi wizara kusimama katika mhimili wakati wa kutekeleza majukumu yake.

‘’Niwashukuru sana wajumbe wa Kamati hii, mmetupa ushirikiano wakati wote wa maboresho ya Kanuni za Madalali na niwaahidi Wizara yangu itasimama katika mhimili wakati wote wa kutekeleza majukumu yake’’ alisema Mhe. Pinda
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akizungumza wakati wizara yake ilipowasilisha Taarifa ya Marekebisho ya Kanuni za Madalali mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo tarehe 19 Januari 2024 jijini Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sheria Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Method Msokele akiwasilisha taarifa ya Marekebisho ya Kanuni za Madalali mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo tarehe 19 Januari 2024 jijini Dodoma.
Sehemu ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo wakifuatilia uwasilishaji Taarifa ya Marekebisho ya Kanuni za Madalali tarehe 19 Jnuari 2024 jijini Dodoma.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo Mhe. Ramadhani Suleiman Ramadhani (Kushoto) akizungumza wakati wa wasilisho la Taarifa ya Marekebisho ya Kanuni za Madalali tarehe 19 Jnuari 2024 jijini Dodoma. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Post a Comment

0 Comments