Ticker

6/recent/ticker-posts

PINDA ATAKA HEKIMA KUSHUGHULIKIA MASUALA YA ARDHI

Na Munir Shemweta, WANMM

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda ametaka hekima itumike katika kushughulikia masuala ya ardhi kwa kuwa idadi ya watu inazidi kuongezeka huku ardhi ikiwa haiongezeki.

Mhe. Pinda ametoa kauli hiyo tarehe 8 Februari wakati akijibu hoja za wabunge katika kikao cha Bunge kujadili Taarifa ya Mwaka ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii katika kipindi cha Februari 2023 hadi Januari 2024.

"Lakini jambo moja ningependa niwaambie watanzania wote, ardhi ya Tanzania kwa ujumla wake haina nyongeza yoyote, tunayo tangu miaka ya hamsini mpaka sasa na haitaongezeka" alisema mhe. Pinda.

Kwa mujibu wa Mhe Pinda, miaka ya hamsini idadi ya watanzania ilikuwa chini ya watu milioni tisa na sasa mwaka 2024 imefikia takriban milioni 61 hivyo ni lazima hekima itumike katika kupitia mambo yanayoongoza sekta ya ardhi.

Amesema, ongezeko la idadi ya watu ni moja ya sababu za kusukumana kwa watanzania katika maeneo yao na amewashukuru wabunge kwa jinsi wanavyochangia mawazo ya jinsi ya kukabili ongezeko la watu bila ongezeko la ardhi.

Katika hatua nyingine Mhe Pinda amesema wizara yake iko mbioni kujenga ofisi za ardhi za mikoa sambamba na kuwa na ofisi za makamishna wa ardhi wasaidizi wa wilaya.

Amesema, kumekuwa na mtengano wa kimawasiliano kati ya maofisa wa wizara ya ardhi kwenye halmashauri walio chini ya wizara na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi mkoa.

‘’tunaenda kuwa na makamishna wa ardhi wa wilaya ili kusimamia halmashauri zilizo chini ya wilaya jambo alilolieleza litasaidia sana kusogeza huduma za sekta ya ardhi karibu na wananchi’’. Alisema Mhe. Pinda

‘’Kuhusu ongezeko la fedha kupitia mkopo wa world Bank ambao moja ya kazi zake ni kufanya maboresho katika eneo la utawala wa wizara. Niwahakikishie waheshimiwa wabunge kuwa, mikoa yote inaenda kupata majengo sambamba na kuanzisha ofisi za ardhi za wilaya ambazo kwa miaka yote haijawahi kutokea’’. Alisema Mhe. Pinda.


Post a Comment

0 Comments