Na Dkt. Mohamed Maguo
Nchi ya Tanzania imejaaliwa na kubarikiwa kuwa na wanawake jasiri, shupavu na shujaa wenye mchango mkubwa katika kukuza na kuimarisha ustawi wa jamii na kuiletea nchi yetu maendeleo. Wanawake ni watu wasiokata tamaa katika maisha na kutokana na hilo huwawezesha kufikia ngazi za juu katika elimu na maisha kwa jumla.
Hayo yamesemwa na Prof. Deus Ngaruko ambaye ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) anayesimamia Taaluma, Tafiti na Ushauri wa Kitaalamu wakati akizungumza na wanafunzi wasichana wa programu ya Foundation mkondo wa sayansi kwenye ukumbi wa OUT mkoani Singida tarehe 27 February, 2024. Akizungumza na wasichana hao amesema:
"OUT ina imani kubwa sana na uwezo wa wasichana katika kufanya vizuri kwenye masomo yao. Ninyi ni wasichana ambao hamkuweza kufanya vizuri katika masomo ya sayansi sekondari na diploma kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukatili wa kijinsia, umasikini, ujauzito, wazazi kutengana nakadhalika. Sasa mmepata fursa hii ya kusoma programu ya Foundation na mkimaliza mtajiunga ngazi ya shahada ya kwanza. Tunawaamini kwamba mnaweza kwa sababu wasichana ni bingwa wa kutokata tamaa katika maisha. Tumieni muda wenu vizuri katika masomo ili asiwepo hata mmoja ambaye atashindwa kufaulu hii foundation. Wizara yetu ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia mradi wa Mageuzi ya Elimu ya Juu kwa maendeleo ya kiuchumi (HEET) imewapatia ufadhili wa asilimia mia moja na hivyo jukumu lenu ni kusoma kwa bidii ili mfaulu muedelee ngazi ya shahada ya kwanza," amesema Prof. Ngaruko.
Aidha, ameongeza kwamba jamii nyingi za Watanzania zimelelewa na wanawake na kufika katika ngazi za juu za elimu na kufanikiwa katika maisha. Akijitolea mfano yeye mwenyewe amesema:
"Mimi binafsi nililelewa na dada yangu ambapo tulikuwa wadogo zake 4. Mara tu baada ya baba yetu kufariki, mimi nilikuwa na umri wa miaka 5 na wakati huo dada yetu alikuwa amemaliza kidato cha Nne na kufaulu kwa daraja la kwanza (division one). Pamoja na ufaulu huo mkubwa lakini hakwenda kidato cha Tano badala yake akajiunga na programu maalumu ya ualimu akawa mwalimu. Lengo lake lilikuwa ni ili aweze kupata kazi ambayo itamwezesha kutulea sisi wadogo zake. Alitulea vizuri na baadae akaolewa na kupata watoto na familia inayomtegemea ikawa kubwa lakini bado aliweza kuimudu.
Baadae alijiendeleza kwa kufanya mtihani wa Mature age entry wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kufanikiwa kufaulu katika kikao cha mara ya tatu. Aliendelea na masomo ya Shahada ya kwanza hapo hapo UDSM na akafaulu kwa daraja la kwanza (first class) na akabakishwa kuwa mhadhiri chuoni hapo.Baada ya muda mfupi alisoma mpaka shahada ya Uzamivu na kuwa Profesa mapema kabisa na kuwapita hata wanaume ambao aliwakuta kama wahadhiri na yeye akiwa mwanafunzi." Ameeleza Prof. Ngaruko.
Kwa hakika, huu ni mfano tosha kwa wanafunzi hao wasichana wa masomo ya Sayansi kuona kwamba nao pia wanayo nafasi ya kufanya vizuri katika masomo na kutokata tamaa kufuatia changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Endelezi (ICE) ya OUT ambao ndio waendeshaji wa mafunzo hayo Dkt. Jacob Leopold ametoa shukurani za dhati kwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo ambaye pia ni mratibu wa HEET wa OUT Prof. Deus Ngaruko kwa kutenga muda kwenda kuzungumza na wanafunzi hao na kuwapatia hamasa ya kufanya vizuri katika masomo. Ameeleza kwamba ICE kupitia kwa wahadhiri wake imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba wanafunzi wanafundishwa vizuri katika mafunzo ya ana kwa ana pamoja na mtandao kwa kuzingatia viwango vyote vya ubora vya OUT na watafanya vizuri katika masomo yao.
Maelezo haya yameungwa mkono na Dkt. Daphina Mabagala ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Ubora cha OUT, kwamba ubora katika utoaji elimu ni kipaombele katika shughuli zote za chuo na watahakisha kundi hili la wasichana wa masomo ya sayansi wanafanikiwa katika masomo yao.
Mafunzo ya ana kwa ana kwa kundi la pili la wasichana wa masomo ya sayansi yanaendelea katika kituo cha OUT Singida ambapo wasichana hao kutoka sehemu mbalimbali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamekutana pamoja na walimu wao. Mfunzo hayo yatadumu kwa kipindi cha wiki mbili na kisha wanafunzi hao watarudi nyumbani na kuendelea na masomo kwa njia ya mtandao.
0 Comments