Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia-WB, wanaendelea na majadiliano ya namna ya utekelezaji wa mradi wa Tanzania ya kidijitali, ambapo wataalam kutoka katika Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Zanzibar pamoja na taasisi mbalimbali za Umma, wamekutana mjini Zanzibar kwa ajili ya majadiliano hayo.
Mradi huo unatarajia kutekelezwa kwa gharama ya dola za kimarekani milioni 150 sawa na shilingi Bilioni 348 za kitanzania na unatazamiwa kuboresha na kuimarisha huduma za mawasiliano nchini.
Ni katika mkutano wa tatu wa kikao cha utekelezaji wa Tanzania ya Kidijitali kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ulioanza februari 19 hadi 23 mwaka huu mjini Zanzibar, ambapo pamoja na mambo mengine, mkutano huo utajadili malengo ya kuongeza upatikanaji wa huduma za mtandao wa intaneti zenye gharama nafuu na ubora wa juu kwa serikali, wafanyabiashara na wananchi sambamba na kuboresha uwezo wa serikali wa kutoa huduma za umma kidijitali.
Akizungumza wakati akifungua mkutano huo, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bi. Khadija Khamis Rajab, amesema matarajio ya serikali ni kwamba miradi ya kimkakati katika sekta ya mawasiliano itatekelezwa.
“Tunatarajia mradi huu utaenda kutekeleza mambo makubwa ili tuweze kutekeleza miradi mingine ya kimkakati katika sekta yetu hii ya mawasiliano, tuna maeneo mengi ya msingi ambayo yatakuwa yamegawanywa katika mradi huu wa Tanzania ya kidijitali, na katika maeneo hayo kutakuwa na maeneo makuu matatu ambayo ni pamoja na kupitia na kuhuisha sheria miongozo na taratibu za kisheria za TEHAMA ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia” amesema Ndugu. Rajab.
Meneja wa mradi huo wa Tanzania ya Kidijitali Bw. Bakari Mwamgugu amesema pia kutakuwa na maboresho ya miundombinu ya TEHAMA, ikiwepo kuunganisha taasisi za serikali katika mkongo wa mawasiliano taifa, kuboresha vituo vya kuhifadhia kanzidata, na kupeleka mawasiliano katika maeneo ambayo hakuna mawasiliano ikiwa ni pamoja na kuboresha mawasiliano kutoka 2G kwenda 4G.
“Lengo la tatu ni kuboresha na kutekeleza mifumo mbalimbali itakayosaidia kutoa huduma bora kwa wananchi na kwa wakati, ukiwepo mfumo wa jamii namba, ambao kila mtanzania atatakiwa kuwa na namba moja tu ya kupata huduma” amesema Bw. Bakari.
Mradi huo una malengo ya kuongeza upatikanaji wa huduma za mtandao wa intaneti zenye gharama nafuu na ubora wa juu kwa serikali, wafanyabiashara na wananchi, sambamba na kuboresha uwezo wa serikali wa kutoa huduma za umma kidijitali.
Mradi wa ‘Tanzania ya Kidijitali' unaofadhiliwa na Benki ya Dunia unatekelezwa kwa usimamizi wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Pamoja na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali zinazohusika na TEHAMA kwa upande wa Tanzania Bara na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
0 Comments