NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk.Dotto Biteko amesema kampeni ya kuhamasisha nishati safi ya kupikia ni ya kila mmoja wetu huku akitoa rai kwa kampuni zinazozalisha mitungi ya gesi kushiriki kikamilifu katika kufanikisha kampeni hiyo.
Amesema Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ndio muasisi wa kampeni hiyo ambapo alizindua mpango wa nishati safi ya kupikia Afrika na kuungwa mkono na watu mbalimbali.
Dk.Bitiko ameyasema hayo Mbagala jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kukabidhi mitungi ya gesi ya Oryx na majiko yake kwa Mama lishe 100 pamoja na majiko banifu, lengo likiwa kuhamasisha nishati safi ya kupikia nchini.
“Mpango huu wa nishati safi Rais wetu Dk.Samia Suluhu Hassan aliuzindua katika mkutano wa kidunia uliofanyika mwaka jana na mwaka huu atahudhuria tena mkutano wa 29 na Rais amekuwa akiifanya kampeni hii ya kuhamasisha nishati safi ya kupikia.
“Kwetu lazima tuweke mkakati maalumu wa kuwafanya wanawake wa Tanzania watumie nishati safi ya kupikia.Tunafahamu ili chakula kiliwe lazima kipikwe na mpishi katika familia zetu ni mama…
“Madhara yanayotokana na nishati chafu mtu wa kwanza kuyapata ni mama.Wanawake wengi wanapata madhara ya kiafya kutokana na matumizi ya nishati isiyo safi,”amesema Dk.Biteko.
Ameongeza katika kutafuta nishati chafu ambayo ni kuni na mkaa watu wengi wamekuwa wakilazimika kuifuata mbali na hivyo kukumbukana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya kubakwa na wakati mwingine kushambuliwa na wanyama wakali ama wadudu kwasababu ya kutafuta nishati hiyo.
Amesisitiza ni wajibu kama taifa kumpatia hadhi mwanamke wa Tanzania sio tu kwa kutamka kwa mdomo wetu bali kwa kuweka mazingira rahisi na gharama nafuu za kupata nishati safi na hivyo itasaidia kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.
“Niwashukuru Oryx kwa kuungana pamoja nasi kwa kutoa mitungi ya gesi kwa mama lishe kwani hiki ni kiashiria kuwa safari ya nishati safi Tanzania imeanza na imeanzia hapa Mbagala, itakwenda na mahali kwingine kwa ajili ya kuwapatia nishati safi wanawake wa Tanzania.”
Amewaomba viongozi wa Serikali pamoja na taasisi kufahamu ajenda ya nishati safi sio ya serikali peke yake bali ni ajenda ya wote, hivyo waisukume kuhakikisha mwanamke wa Tanzania anapata hadhi.
“Ni matumaini mitungi hii ya gesi ambayo tumeigawa leo itakuwa ni chachu ya kuchochea nishati safi ya kupikia.Hivyo niendelee kuziomba kampuni nyingine zinazozalisha mitungi ya gesi ama nishati nyingine yasibaki nyuma.Wafanye kila wanaloweza kuhakikisha wanawake wa Tanzania wanapata nishati safi na wanapata maendeleo.”
Awali Mkurugenzi wa Oryx Gas Benoite Araman amesema Oryx Gas Tanzania inajipongeza kwa kujulikana kuwa kampuni kinara katika usambazaji wa gesi ya LPG kwa Watanzania kwa sasa na kwamba wataendelea kuwekeza zaidi katika kuratibu kubadilisha na kueneza nishati safi kutumika na Watanzania kwa kutumia gesi ya Oryx kwa manufaa yetu wote.
“Nawaomba kuwahimiza wote hapa kutumia gesi ya LPG katika shughuli zenu mbalimbali ili kuleta maendeleo katika nchi yetu pendwa na kwa ajili ya kuboresha Maisha yetu kiujumla. Tunafurahi kumkabidhi mitungi ya gas mia saba (100) kwa ajili ya wakazi wa Mbagala Zakheim.”
Aidha amesema kupika kwa gesi ya Oryx ni kulinda mazingira kwa kuacha kukata miti huku akisisitiza zaidi ya yote ni kulinda afya ya wanawake kwa kuwaepusha kuvuta moshi na mvuke unaoathiri mapafu na afya yao unaotokana na kuni na mkaa.
“Wanawake wanatumia muda mchache kupika hivyo wanapata nafasi kufanya shughuli nyingine za maendeleo na kuepuka kugombana na wenza wao kwa kuchelewesha chakula, na wanaume pia watajiongezea marks ukiwazadia wamama mitungi ya gesi.Kwa kutumia gesi ya Oryx, Watoto wanakua na muda mwingi zaidi kusoma na sio kwenda kutafuta kuni,”amesema Benoit.
0 Comments