Ticker

6/recent/ticker-posts

KAMATI YA BUNGE YATEMBELEA UJENZI WA JENGO JIPYA LA DAWASA YETU

Kamati ya Kudumu ya Bunge Uwekezaji na Mitaji ya Umma imekagua na kufurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya la DAWASA Yetu lililogharimu shilingi bilioni 48.9 na linatarajiwa kukamilika mwezi June mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua mradi wa jengo hilo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Deus Sangu amesema kuwa Kamati imejionea utekelezaji mzuri wa mradi huu wa ujenzi wa jengo kwa ufanisi na kwa ubora.

Amesema kuwa kupitia jengo hili, DAWASA ambayo ni Mamlaka kubwa nchini ya maji litasaidia kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma ya Majisafi kwa wananchi wa Dar es Salaam na Pwani.

Mhe. Sangu ameipongeza Serikali ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuzingatia umuhimu wa kazi kubwa waliyonayo DAWASA ya kuhudumia majimbo 16 ya uchaguzi na mikoa minne ikiwemo Dar es Salaam, Pwani, baadhi ya maeneo ya Morogoro na Tanga, na kuamua kutoa fedha za kujenga jengo hili la kisasa.

"Niipongeze Serikali kwa ushirikiano mkubwa walioutoa kwenye utekelezaji wa mradi huu," ameeleza Mhe Sangu.

Ameongeza kwa kuipongeza DAWASA kwa kuongeza ubunifu kwa kufunga mifumo ya kufuatilia upotevu wa maji na miundombinu ya maji kwenye maeneo ya huduma, na hii imekuwa ni changamoto kubwa kwenye Mamlaka nyingi kunakosababishwa na kutokuwa na mifumo sahihi ya kufuatilia upotevu wa maji. Hivyo hatua hii ya DAWASA ni mfano wa kuigwa.

Amebainisha kuwa Kamati imewasihi DAWASA kuongeza nguvu na kupunguza upotevu wa maji kutoka asilimia 37 ya sasaa mpaka kiwango kinachopendekezwa kimataifa cha asilimia 20 ili kuboresha huduma kwa wananchi wote.

Mbali na hapo Mwenyekiti wa Kamati ameipongeza Mamlaka kwa kuweza kuongeza wigo wa utoaji wa huduma kutoka wateja laki 2 mpaka wateja 432000 ndani ya kipindi cha miaka mitatu.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi DAWASA Ndugu Laston Msongole ameishukuru Kamati ya Bunge kwa kutembelea mradi huu na kujionea maendeleo ya jengo letu na hatua ilipofikia.

"Wamejionea na wameridhika na kazi iliyofanyika pamoja na kuona thamani ya fedha iliyowekweza imeleta tija, tunawaahidi kukamilisha sehemu iliyobaki ndani ya wakati," ameeleza Ndugu Msongole.

Post a Comment

0 Comments