Na Munir Shemweta, BABATI
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda amewatuliza wananchi wa vijiji vya Kimara na Kiru Dick vilivyopo halmashauri ya Babati mkoa wa Manyara kufuatia mgogoro wao na wawekezaji wa mashamba.
Hatua hiyo inafuatia wananchi wa vijiji hivyo kuingia kwenye mgogoro mkubwa na wamiliki wa mashamba ya Miombo Estate na Hamir Estate yaliyopo Bonde la Kivu katika halmashauri ya Babati mkoa wa Manyara.
Aidha, uamuzi huo ni utekelezaji wa maagizo ya Katibu Mwenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Paul Makonda ambaye katika ziara yake mkoani Manyara aliwasilishiwa malalamiko kuhusu mgogoro huo na kumuelekeza Naibu Waziri Pinda kwenda kutafuta suluhu.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji hivyo tarehe 4 Machi 2024 wilayani Babati akiwa katika ziara yake ya siku mbili mkoani Manyara, Naibu Waziri wa Ardhi amewataka wananchi wa vijiji hivyo kuwa watulivu wakati serikali ikiendelea kushughulikia mgogoro huo.
‘’Kwa hiyo ninachokuja kuwaambia nyie, kwanza ni utulivu na kitu kikubwa kitakachotutawala katika hili ni utulivu na kwa jinsi tunavyokwenda kukubaliana mnakwenda kupata maeneo mtakayoweza kwenda kuendesha maisha yenu’ alisema Pinda
Amewakumbusha wananchi wa vijii vilivyoingia kwenye mgogoro kuwa, wasisahau kwamba uwepo wa wawekezaji kwenye maeneo hayo bado ni halali hivyo wakati serikali ikienda kuweka mambo sawa basi waepuke ushabiki.
‘’Kwenye kipindi hiki ambacho tunakwenda kuyaweka mambo haya vizuri ushabiki hautakiwi na lazima hekima iwatangulie. Tusipokuwa na hekima katika kutekeleza jambo hili bado kutakuwa na mgongano ikiwemo kesi’’ alisema Mhe, Pinda.
Kwa mujibu wa Mhe, Pinda, ujio wake katika kutafuta suluhu ya mgogoro huo wa mashamba wilayani Babati ni kusimamisha yale masuala ya kesi kwa zile pande zinazopingana ili zikae meza moja na kumaliza mgogoro kwa lengo la wananchi kuishi kwa amani.
Awali wananchi wa vijiji hivyo walimueleza Mhe, Pinda kuwa, wakati wa kutafuta suluhu ya mgogoro huo ahakikishe makubaliano makubwa ni makazi ya watu kutoguswa sambamba na wao kutambuliwa kwa kuwa wamezaliwa na mababu zao waliokuwa wakiishi maeneo hayo.
‘’Tunashauri kwamba nyumba za watu katika mgogoro huu unaokwenda kutatuliwa ziangaliwe kwa busara, tuangalie makazi ya watu yasiguswe na mgogoro huu tena’’ walisema
Aidha, wamemshukuru Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Pinda kwa kwenda katika vijiji hivyo kutafuta suluhu ya mgogoro huo ambapo wametaka mgogoro huo kumalizwa viziuri ili wananchi waishi vizuri na wawekezaji.
Kwa upande wao wawekezaji wa mashamba ya Miombo na Hamir Estate wamemueleza Mhe, Pinda kuwa hawana nia mbaya na wananchi wa vijiji vinavyowazunguka na kueleza kuwa, hata uamuzi wao wa kuachia sehemu ya maeneo ya mashamba yao wanayomiliki ni kutaka kuishi kwa amani na kuepuka ugomvi na wananchi.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda (kulia) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kiru Dick katika halmashauri ya Babati mkoa wa Manyara alipokwenda kutafuta suluhu ya mgogoro wa ardhi baina ya wananchi na mmiliki wa shamba la Hamir Estate tarehe 4 Machi 2024.
Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Kimara katika halmashauri ya Babati mkoa wa Manyara wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda (hayupo pichani) alipokwenda kutafuta suluhu ya mgogoro wa ardhi baina ya wananchi na mmiliki wa shamba la Miombo Estate tarehe 4 Machi 2024.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda (Kulia) akiagana na mmoja wa wananchi katika kijiji cha Kimara mara baada ya kumaliza kikao cha kutafuta suluhu ya mgogoro wa ardhi baina ya wananchi na mmiliki wa shamba la Miombo Estate tarehe 4 Machi 2024. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
0 Comments