Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) limefanikisha kufungwa kwa mtambo unaoondoa ganda laini la korosho ili kuongeza thamani zao hilo kabla ya kusafirishwa.
Akizungumza leo Machi 29,2024 wakati wa kusaini makubaliano na makabidhiano ya mtambo huo kwa Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (Camartec), Mkurugenzi Mkuu wa Tirdo, Profesa Mkumbukwa Mtambo, amesema lengo ni kuongeza thamani zao hilo kabla ya kusafirishwa.
Amesema walipewa jukumu la kuleta mitambo itakayoondoa ganda laini la korosho kukamilisha mnyororo mzima wa ubanguaji korosho.
Taasisi zingine zilizofanikisha kufungwa kwa mtambo huo ni Shirika la Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (Temdo) na Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (Sido).
"Tunaishukuru serikali kwa kuziwezesha taasisi zetu kifedha na kuweza kupata mitambo kama hii," amesema Profesa Mtambo.
Kwa upande wake Mhandisi Atupele Kilindu kutoka Idara ya Uhandisi Maendeleo Tirdo, amesema mtambo huo uliogharimu Sh milioni 40 una uwezo wa kuondoa ganda laini kilo 350 kwa saa.
Amesema lengo ni kuanzisha kiwanda cha mfano kwa ajili ya kufundisha wajasiriamali namna ya ubanguaji na kuongeza mnyororo wa thamani katika zao la korosho.
Kaimu Mkurugenzi wa Camartec, Mhandisi Paythias Ntella, amesema tayari wana kiwanda darasa cha kubangua korosho kilichoanzishwa na kituo hicho wilayani Manyoni mkoani Singida.
Amesema kiwanda hicho kimeanzishwa kwa lengo la kuwasaidia wakulima kubangua korosho na kuacha kuuza zikiwa ghafi na kushindwa kunufaika na kilimo hicho.
"Tunafundisha wajasiriamali katika hatua zote ili kubangua na kumenya ili vitengenezwe viwanda vingi zaidi sehemu nyingine," amesema Ntella.
Lengo la Serikali kuhakikisha asilimia 60 ya korosho zote zinazozalishwa nchini zinabanguliwa ifikapo msimu wa mwaka 2025/26 na asilimia 100 ifikapo mwaka 2030.
0 Comments