Ticker

6/recent/ticker-posts

Waadhimisha siku ya wanawake kwa kupanda miti Bwawa la Kwamaizi kulinda vyanzo vya maji

Kufuatia maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani yanayofanyika Machi 08 kila mwaka, wanawake wa kata ya Kideleko katika halmashauri ya mji wa Handeni wametumia nafasi hiyo kupanda miti na kufanya usafi katika bwawa la maji la Kwamaizi katika bwawa la maji la Kwamaizi lililopo kata hiyo ili kuendelea kulinda vyanzo vya maji.

Akizungumza katika maadhimisho hayo Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi Mradi wa Handeni Trunk Main, Yohana Mgaza amesema

toka kuzinduliwa kwake mwaka jana, bwawa la Kwamaizi limekua ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa kata ya Kideleko hasa wakinamama ambao wao ndio wana jukumu la kutafuta maji kila siku.

Amesema kutokana na umuhimu wa bwawa hilo waliona ni vyema kutumia siku hiyo kulishafisha na kupanda miti rafiki kuzunguka bwawa hili ili liweze kudumu katika muda uliokusudiwa.

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Shirika la WaterAid Tanzania, Neema Kimaro amesema bwawa la Kwamaizi katika halmashauri ya Handeni lilikamilishwa chini ya Ufadhili wa Kampuni ya bia ya Serengeti na kusimamiwa na WaterAid ambapo tangu kukamilika kwake mwaka jana linahudumia takribani wananchi 1944.

Aidha akizungumzia nafasi ya kinamama katika usimamizi wa miradi ya maji na usafi wa mazingira, Kimaro amesema licha ya mradi huo kulenga huduma ya maji safi kwa wananchi, pia, kuliundwa kikundi maalum cha wakina mama 24 waliosajiliwa kwa kazi maalum ya kuwezesha jitihada za kusimamia maswala yote ya uhifadhi wa mazingira na ulinzi wa miundombinu ya maji ikiwemo usafi katika bwawa.

"Kikundi hiki kitafanya majukumu yake kwa kushirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira – HTM wakiratibiwa na kusimamiwa na Halmashauri ya Mji wa Handeni.” amesema

Mara baada ya kumaliza zoezi la upandaji miti katika bwawa hilo, mnufaika na Mwenyekiti wa kikundi cha kinamama wanaosimamia mradi huo alimalizia kwa kusema, Fransisca Mhando amesema“Lengo la hiki kikundi chetu cha kinamama ni kusimamia mauzo ya maji katika hili bwawa ila pia kusimamia matunzo na usafi wa mazingira kwa ujumla katika eneo linalozunguka bwawa.

Nchini Tanzania kaulimbiu ya maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani ni “Wekeza katika wanawake: Kuharakisha maendeleo”

Post a Comment

0 Comments