Ticker

6/recent/ticker-posts

LSF YATIA SAINI PAMOJA NA BENKI YA STANBIC TANZANIA KULETA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI WA KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO

Jumatatu, Aprili 29, 2024 - Dar es Salaam, Taasisi isiyo ya kiserikali ya The Legal Services Facility (LSF), kwa kushirikiana na Benki ya Stanbic Tanzania, zimesaini makubaliano ya ushirikiano wa kutekeleza miradi ya maendeleo yenye lengo la kuwainua wanawake na wasichana kiuchumi, kielimu na kiafya.

Mkataba huu wa miaka miwili unalenga katika kuweka juhudi na rasilimali za pamoja kati ya taasisi hizi ili kukabiliana na changamoto za kijamii, hasa zinazowakabili wanawake na wasichana.

Makubaliano haya yanalenga zaidi katika kuweka mazingira mazuri ya elimu na kuboresha afya ya uzazi pamoja na kuwawezesha wanawake kupata fursa za kiuchumi, elimu ya kifedha, pamoja na kuwaunganisha kwenye fursa za kupata mitaji kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi.

Lengo kuu la mashirikiano hayo ni kuhakikisha fursa sawa, kukuza usawa wa kijinsia, na uwezeshaji wa wanawake, hivyo kuwawezesha kutimiza ndoto zao.

Maeneo haya yanawiana kati ya vipaumbele vya benki hususan katika miradi yake ya kijamii Pamoja na dhamira ya LSF ya kukuza haki ya kijamii kwa maendeleo endelevu.

Aidha mashirikiano haya yatachangia moja kwa moja katika kufanikisha kipaumbele cha Taifa na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs); 5 (Usawa wa Jinsia), 3 (Afya Bora na Ustawi), 4 (Elimu ya Ubora), na 16 (Amani, Haki, na Taasisi Imara. )

Akiongea wakati wa utiaji saini Mkataba huo Mkurugenzi Mtendaji wa LSF, Bi.Lulu Ng’wanakilala alisema, “Tunajivunia kusaini mkataba huu leo ​​ambao unatilia mkazo dhamira yetu ya kuwakutanisha wadau hususani mashirika binafsi ili kuunga mkono juhudi za pamoja katika kutatua changamoto za jamii kwa njia inayoleta tija na matokeo endelevu. Makubaliano haya tunaoingia leo yatarahisisha utekelezaji wa miradi ya pamoja na kukuza fikra shirikishi katika kuweka miradi na mipango mipya pamoja na kuendeleza yale ambayo yalishawekwa kabla. Kwa hivyo, nachukua fursa hii kuishukuru Benki ya Stanbic kwa kushirikiana nasi.Napenda hasa kuwashukuru kwa mradi wa elimu na afya ya uzazi, ambao utatekelezwa kupitia mbio za kila mwaka za Run for Binti. Tunayofuraha kuwa na mshirika muhimu katika mbio za mwaka huu. Kupitia ushirikiano huu, tunaamini kabisa kuwa tunaweza kufikia walengwa zaidi kuliko hapo awali.”

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Benki ya Stanbic Bw.Manzi Rwegasira alisema, “Tuna furaha kubwa kushirikiana na LSF ili kufanikisha miradi itakayowezesha vijana na wanawake katika jamii kote nchini, pamoja na kukabiliana na athari za mazingira kwa kupanda miti ili kuchangia malengo ya nchi yetu yaTanzania katika kulinda mazingira.

Ushirikiano huu unalenga kuimarisha fursa za kiuchumi kwa wanawake na vijana kupitia mipango inayozingatia ujuzi wa kifedha na maendeleo ya biashara. Ili kuwezesha kuimarisha ujuzi kwa walengwa, tunalenga kutoa rasilimali zinazohitajika katika kuleta uhuru na mafanikio endelevu ya kifedha.

“Tuna furaha kufanya kazi pamoja na LSF haswa katika kuendeleza mipango hii, ambayo inachangia moja kwa moja katika mipango ya maendeleo endelevu ya nchi yetu. Tunatazamia kuleta matokeo chanya na endelevu kwenye maisha ya wanawake, vijana, na jamii zote za Tanzania.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Stanbic, Manzi Rwegasira, na Mkurugenzi Mtendaji wa LSF, Lulu Ng’wanakilala, wakisaini makubaliano ya ushirikiano yaliyolenga kuwawezesha wanawake na wasichana, kiuchumi , kiafya, kielimu. Aidha, ushirikiano huu unalenga kushughulikia masuala ya mazingira kwa maendeleo endelevu.
Mkurugenzi Mtendaji wa LSF, Lulu Ng’wanakilala na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Stanbic, Manzi Rwegasira wakibadilishana mikataba mara baada ya kusaini.

Post a Comment

0 Comments