Na Mwandishi Wetu
WAKATI Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana akitarajiwa kuanza ziara Aprili 14, 2024 tayari kuna mtafaruku kwa makada wa Chama hicho tawala wilayani Rorya.
Hatua ya kuibuka kwa hali hiyo inatokana na uamuzi unaodaiwa kufanywa na baadhi ya viongozi wa Chama na Serikali kuzuia makundi mengine kutomuona kiongozi huyo atakapokuwa katika ziara hiyo na kueleza hali hali mambo yanayoendelea kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Vijiji, Mitaa na Vitongoji unaotarajiwa kufanyika mwaka huu pamoja na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.
Kinana na msafara wake wanatarajiwa kuanza ziara ya kikazi Aprili 14, mwaka huu mkoani humo kwa lengo la kusikiliza kero na kuzipatia ufumbuzi pamoja na kusikiliza na kutoa maagizo ya chama kuelekea uchaguzi.
Baada ya taarifa ya ziara hiyo, baadhi ya makada wa CCM wilayani Rorya wameibuka leo Aprili 12, 2024 jijini Dar es Salaam na kueleza kero ambazo wanataka Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Bara kuzishughulikia anapokuwa wilayani humo ikiwamo kujua hali ya mambo yanayodaiwa kufanywa na baadhi ya viongozi wa chama na Serikali wilayani humo..
Akizungumza na waandishi wa habari Kada wa CCM wilayani Rorya, Baraka Otieno, amedai kero kubwa ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya kuwagawa wanachama kwa kuzungumza lugha ya Kijaluo kwenye vikao halali vya chama.
Amesema pia baadhi ya viongozi wa CCM kutoka kata mbalimbali kusimamishwa kazi kutokana na sababu ambazo hazijabainika na kuibuka makundi ya kuwagawa wanachama wa CCM kutoka katika Kata ya Subi kuwa Subi 1 na Subi 2.
Pamoja na hiyo alimtaja Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka na amedai kwamba ameshindwa kusimamia vyema suala la ulinzi na sulama na kusababisha mifugo zaidi ya 100 kuibiwa katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, kuachia wezi waokamatwa na kutotatua kilio cha wananchi wanaodai fidia kwenye shamba la mifugo la Utengi.
Kutokana na hali hiyo amemuomba Kinana kwenda na kusikiliza kilio cha wananchi hao na ikiwa viongozi wa CCM watashindwa kumueleza hilo yeye amejiandaa kukabidhi hoja hiyo kwa maandishi kwa kiongozi huyo wa CCM.
“Tunajua wakati haya yakienelea na kupitia ziara hiii ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, tunapenda pia ajie Roya haina utulivu chama kinaendeshwa pasipo utaratibu ikiwamo viongozi kusimamishwa kisa tu hila za uchaguzi, jambo hili si sawa sisi wana Rorya na wana CCM ni wajibu wetu kusema ukweli.
“Ukienda upande wa Serikali Mkuu wa Wilaya, ameshindwa kusimamia kabisa suala la ulinzi na usalama kwani watu wanaibiwa na hata kuporwa ng’ombe wao kwa nguvu na kuvushwa kwenda nchi jirani.Hawana msaada wowote wa Serikali zaidi ya DC naye kujiingiza kwenye siasa hali ya kuwa si kazi yake.
“Rais Samia na wadau wa maendeleo wana mapenzi ya dhati na Wilaya yetu ya Rorya lakini bahati mbaya tumekosa viongozi wenye ubunifu na wenye kuwasaidia wananchi na badala yake wana kazi ya kubeba ajenda zao binafsi kuelekea uchaguzi na kuumiza watu,” amesema Otieno.
Alipotafutwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rorya, Ongujo Wakibara kwa njia ya simu ili kuzungumzia tuhuma hizo alikanusha kuwapo kwa makundi kati ya Kata ya Subi 1 na Subi 2 pamoja na kuzungumza kilugha kwenye vikao vya chama licha ya kudai tarafa tatu kati ya nne kuzungumza lugha ya Kijaluo.
Kuhusu viongozi wa chama hicho waliosimamishwa kazi, alithibitisha kuwa ni wanne na hatua hizo zimechukuliwa na ofisi za CCM Mkoa wa Mara, baada ya wilaya kupeleka mapendekezo yaliyohusu makosa yao ambayo hata hivyo hakuyataja.
“Tunaomba Kinana anapofika Rorya kusikiliza kero za wananchi na wanachama wana kero ambazo viongozi wetu ndio wanaozifumbia macho na kuzuia kwa maslahi yao binafsi, tunataka waseme kama wataona ni sahihi kufanya hivyo,” amesema Wakibara.
Kuhusu madai ya kusimaishwa kwa viongozi hao wa CCM hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi wa Vijiji, Mitaa na Vitongoji haoni kama inaathiri mshikamano, amejibu suala hilo ni la kawaida kwani chama kina timu kubwa ya watu ambao wanaweza kufanyakazi hiyo.
“Kwa mfano wewe ukiiba na ukasimamishwa kazi kwani nafasi yake hakuna wa mtu wa kujaza…Sasa hilo si jambo la kushangaza ndani ya chama chetu. Sijasema kuwa wameiba ila wamesimamishwa kwa sababu ambazo uongozo wa Mkoa unaweza kuzisema lakini si mimi,” amesema Wakibara
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka akizungumzia kwa njia ya simu na waandishi wa habari, amesema suala la usalama wa mifugo ni tatizo linalotokana na wananchi wengi wa wilaya hiyo kushindwa kujenga mazizi na usalama mdogo wa mifugo na kukanusha kuachia mwizi wa mifugo kwa amri yake.
“Siwezi kumtetea mwizi, mwizi ni mhalifu tu. Mifugo inalala nje, imefungwa kamba laini na hakuna ulinzi ndio sababu inaibiwa. Tumeanzisha kampeni ya 'Ng'ombe zizini' kama ni ng'ombe ni mmoja au wawili mfugaji aonyesha unapofugia, tumeanzisha na kampeni ya ulinzi shirikishi kila vijana saba kutoka katika kila kitongoji washiriki ili kumaliza tatizo hili,” amefafanua Chikoka.
Kuhusu suala la wananchi wa shamba la mifugo la Utengi kutolipwa fidia, amesema ni suala la kisheria na taratibu za kuwalipa zinafuata na hawawezi kufanya uamuzi wowote bila kufuata taratibu.
0 Comments