Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imekita kambi katika Viwanja vya Bunge Dodoma kueleza kuhusu shughuli za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini kwa Waheshimiwa Wabunge.
Kupitia Maonesho ya Wiki ya Nishati 2024, PURA inaeleza masuala mbalimbali yakiwemo hatua zilizofikiwa katika utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini na hali ya uzalishaji wa gesi asilia kutoka katika vitalu vya Songo Songo na Mnazi Bay.
PURA pia inatumia maonesho hayo kueleza mipango iliyopo kunadi vitalu vilivyowazi vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia na suala zima la udhibiti wa shughuli za mkondo wa juu wa petroli.
Maonesho ya Wiki ya Nishati yanaratibiwa na Wizara ya Nishati na yamefanyika kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2022.
Kwa mwaka huu, Maonesho hayo yanafanyika Aprili 15 hadi 19, 2024 katika Viwanja vya Bunge - Dodoma.
Maonesho ya Wiki ya Nishati yanatoa fursa kwa Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufahamu kwa kina kuhusu miradi na programu mbalimbali zinazotekelezwa katika sekta ya nishati nchini.
Afisa Sheria Mwandamizi kutoka PURA, Bw. Abbas Kisuju (kushoto) akielezea shughuli za mkondo wa juu wa petroli kwa Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Mwakiposa Kihenzile wakati wa Maonesho ya Wiki ya Nishati 2024.
Mjiolojia kutoka PURA, Bw. Ebeneza Mollel (kushoto) akielezea shughuli za mkondo wa juu wa petroli kwa Mhe. Mansoor Shanif Jamal, Mbunge wa Jimbo la Kwimba wakati wa Maonesho ya Wiki ya Nishati 2024.
Mjiolojia kutoka PURA, Bw. Said Chamba (kushoto) akielezea shughuli za mkondo wa juu wa petroli kwa Mhe. Aida Khenani Mbunge wa Nkasi Kaskazini wakati wa Maonesho ya Wiki ya Nishati 2024.
0 Comments