Na Aisha Malima-Morogoro
Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Morogoro inaendelea na kazi ya kuziba mashimo na kukarabati barabara kuu ya Morogoro – Iringa ikiwemo katika eneo la Kobogwa lilipo katika hifadhi ya Taifa ya Mikumi ambapo kumetokea shimo kubwa baada ya maji kupita pembezoni mwa Kalvati.
Akizungumza na Kipindi cha TANROADS Mkoa kwa Mkoa leo tarehe 26 Aprili 2024; Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro Mhandisi Alinanuswe L. Kyamba amesema kuwa tayari Mkandarasi yupo eneo hilo akiendelea na kazi ambapo mpaka kufika leo usiku kazi hiyo utakuwa imemalizika.
"Mvua zimeendelea kunyesha bila kukatika na jitihada zinaendelea kufanyika kila siku, eneo hili ambalo limeleta taharuki katika barabara hii ya Mikumi. Mashimo yametokea juzi, tukayaziba kidharura lakini unapoziba kidharura mvua zikinyesha tena zinaondoa ule mchanga ambao tumeuweka kwa sababu kipindi hiki cha mvua huwezi kuziba na lami, lami haikubali kipindi cha mvua mpaka jua liwake" Amekaririwa Mhandisi Kyamba na kusisitiza kuwa
“Tunaendelea na kazi ya kuziba mashimo yote kwenye barabara hii kuanzia Msamvu - Mikumi hadi Iringa mpaka tuyamalize kutokana na mvua kubwa kila siku mashimo yanajitokeza juzi hapa kwenye hili Kalvati maji yamepita pembeni yametengeneza shimo kubwa hapa katikati tukaanza kuleta mitambo na nyenzo za kazi, kwa sasa barabara inapitika upande mmoja na upande mwingine kazi inaendelea’’
Kwa upande wake Mhandisi Aloyce Stephen kutoka Kampuni ya Kizawa ya CGI Contractor Ltd inayofanya kazi hiyo amesema kazi imeendelea kufanyika bila kusababisha msongamano wa magari na matarajio ni kwamba magari yaemdelee kuruhusiwa kupita pande zote za barabara bila tatizo lolote.
Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa fursa na kuwajali Wakandarasi wazawa ikiwa ni pamoja na kuwapa malipo ya kazi kwa wakati jambo ambalo linawapa nguvu ya kuwa tayari kutekeleza majukumu yao wakati wote hata kwenye kazi za dharura kama hizo.
0 Comments