Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoani Katavi imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kufanya kazi ya matengenezo na kurejesha miundombinu ya barabara na madaraja yaliyosombwa na maji ya mafuriko ya mvua kubwa za El-nino zilizonyesha kwa wingi mkoani humo tarehe 14 na 15 Aprili 2024.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Katavi Martin A. Mwakabende amesema kufuatia uharibifu huo Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imepeleka kiasi cha shilingi bilioni 1.1 mkoani humo kwa ajili ya kazi ya matengenezo ya dharura ya miundombinu iliyoharibika.
Ameyasema hayo tarehe 7 Mei 2024 baada ya kutembelea na kukagua maeneo yaliyopata athari; ambapo amemshukuru na kumpongeza Mhe. Rais Dkt. Samia kwa namna ambavyo ameuwezesha Mkoa wa Katavi kwa kuupatia kiasi hicho cha fedha ambacho kimesaidia kuhakikisha kazi ya matengenezo miundombinu hiyo inakamilika kwa wakati.
“Pia tunamshukuru Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa kwa namna ambavyo ameweka msukumo kuhakikisha kazi hii inakamilika, vile vile nampongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Balozi Mha. Aisha Amour, Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mha. Mohamed Besta na Viongozi wengine kwa namna ambavyo wametuongoza kufikia malengo ya kurudisha huduma kwa watumiaji wa Barabara ndani ya Mkoa wa Katavi’’a meeleza Mha. Mwakabende.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Matengenezo TANROADS Katavi Mha. Aumsuri Jacob ametaja maeneo yaliyoathirika ni Barabara ya kutoka Kathuila kwenda Karema umbali wa kilomita 12 ambapo barabara iliharibika na kukata kabisa mawasiliano kila upande.
Maeneo mengine ni daraja la misunkumilo, Daraja la Stalike, Daraja la mirumba na Kilida ambapo kazi ilifanyika ndani ya siku mbili na kurejesha miundombinu yote katika hali ya kawaida.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Mipango TANROADS Katavi Mha. Happyness Benjamin Chaji amesema kwa sasa miundombinu yote inapitika bila shida na wamejipanga kuhakikisha katika bajeti ijayo ya mwaka wa fedha 2024/2025 fedha ambayo inatolewa na Serikali inapelekwa kwenye maeneo husika ili kutekeleza mipango iliyowekwa na kuwezesha miundombinu yote kupitika wakati wote.
0 Comments