Ticker

6/recent/ticker-posts

AIR TANZANIA KUONGEZA SAFARI ZA KIMATAIFA

Katika kutanua wigo wa safari zake za kimataifa, Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) iko kwenye maandalizi ya kuanzisha safari za moja kwa moja kuelekea Muscat nchini Oman.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) Mhandisi Ladislaus Matindi alisema haya baada ya kukutana na Balozi wa Oman nchini Mhe. Saud bin Hilal Alshaidani tarehe 26 Juni 2024 katika Ofisi za Ubalozi zilizopo jijini Dar es Salaam.

"Taratibu za kufungua kituo nchini Oman zimeanza ambapo Air Tanzania tumeshampata wakala mkuu wa mauzo ya tiketi zake nchini Oman (General Sales Agent), tumeteua Msimamizi wa Kituo hicho" alisema Mhandisi Matindi na kuongeza kuwa kwa sasa hatua iliyofikiwa ni kukamilisha uandaaji wa timu ya marubani, ndege itakayotumika pamoja mpangilio wa safari.

Balozi wa Oman nchini Tanzania, Saud bin Hilal Alshaidani alisema mazungumzo yake na Air Tanzania yamekuwa na tija ambapo wamejadili fursa zilizopo kwa kutumia ndege za abiria na mizigo.

"Kwa idadi kubwa ya raia wa Oman waliopo hapa nchini, biashara kati ya nchi hizi mbili ikiendelea kukuzwa, ni matarajio yangu kuwa Air Tanzania itanufaika na fursa hii pasi na mshindani bali mshirika kwa upande wa abiria na mizigo", alisema Mhe. Balozi Alshaidani na kutaja mazao matatu yanayoweza kuwekewa msisitizo.

“Tunaweza kujikita kwenye usafirishaji wa aina tatu tu za matunda zenye uhitaji mkubwa nchini Oman, maembe, nanasi na parachichi. Hii itanufaisha pande zote, wafanyabiashara wa Tanzania na Oman”.

Kwa sasa Air Tanzania inafanya safari za ndani na nje ya nchi. Kwa safari za kikanda na kimataifa ina safari za Dubai (UAE), Mumbai (India), Guangzhou (China), Bujumbura (Burundi), Entebbe (Uganda), Hahaya (Comoro), Harare (Zimbabwe), Lusaka na Ndola (Zambia), Nairobi (Kenya) na Lubumbashi (Congo). Kwa Tanzania ATCL imekuwa ikifanya safari zake kati ya Dar es salaam kwenda mikoa ya Dodoma, Mwanza, Mbeya, Kilimanjaro, Arusha, Songea, Katavi, Zanzibar, Mtwara, Tabora na Kigoma.
Balozi wa Oman nchini Tanzania Mhe. Saud bin Hilal Alshaidani (kulia) akimueleza Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania Mha. Ladislaus Matindi namna wanavyoweza kushirikiana kibiashara kwa nchi hizo mbili.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania Mha. Ladislaus Matindi akimkabidhi Jarida la Twiga linalotumika ndani ya ndege hizo Balozi wa Oman nchini Tanzania Mhe. Saud bin Hilal Alshaidani (kulia) baada ya mazungumzo kuhusu kukuanzisha safari za Oman.

Post a Comment

0 Comments