Ticker

6/recent/ticker-posts

FRIENDS OF SERENGETI YATOA UFADHILI WA VIFAA VYA DORIA VYENYE THAMANI YA ZAIDI YA TZS. MILLIONI 40 KWA ASKARI WA UHIFADHI WA TAWA

Na Beatus Maganja, Arusha.

Katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhifadhi na kulinda rasilimali za wanyamapori nchini ikiwa ni pamoja na kudhibiti wa wanyama wakali na waharibifu, Marafiki wa Serengeti Uswisi "Friends of Serengeti Switzerland" wametoa msaada wa mahema 20, mabegi ya kulalia "Sleeping bags" 20 yenye thamani ya Shillingi Millioni thelathini laki tisa na elfu arobaini (30,940,000/=) pamoja na Lita 2,120 za mafuta ya gari zenye thamani ya Shillingi Millioni Saba (7,000,000/=) kwa ajili ya kusaidia shughuli za doria kwa Askari wa TAWA Kanda ya Kaskazini.

Akimkabidhi Kaimu Kamanda wa Uhifadhi TAWA Kanda ya Kaskazini Privatus Kasisi msaada huo Katika Ofisi za Kanda zilizopo jijini Arusha Juni 09, 2024, Bi Suzan Peter Shio Kwa niaba ya bodi ya Marafiki wa Serengeti Uswisi amesema lengo na shabaha yao ni kusimamia uhifadhi wa mazingira na wanyamapori ili kuhakikisha Tanzania inakuwa katika hali yake ya uasili kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.

"Tumekuwa tukifanya shughuli za ufadhili wa uhifadhi kwa miaka kadhaa nchini Tanzania, na kwa TAWA tumeanza zaidi ya miaka 10 iliyopita (tangu ikiwa Idara ya Wanyamapori) na hasa tulijikita kwenye ufadhili wa mafuta kwa ajili ya kuwasaidia Askari kufanya doria" amesema

Aidha Bi Suzan ameishukuru TAWA kwa ushirikiano inayoendelea kuutoa kwa wadau hao na kukiri kuwa ushirikiano huo umekuwa chachu ya kuwapa moyo wa kuendelea kuwafadhili.

Naye Kaimu Kamanda wa Uhifadhi TAWA Kanda ya Kaskazini Privatus Kasisi ameishukuru bodi ya Marafiki wa Serengeti kwa ufadhili huo ambao unalenga kuboresha usimamizi wa shughuli za uhifadhi na ulinzi wa rasilimali za wanyamapori hususani katika kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu katika Kanda yake anayoisimamia.

"Sisi kama TAWA tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa bodi ya Marafiki wa Serengeti Uswisi ambao wamekuwa wakitusaidia misaada mbalimbali kwa ajili ya kusimamia uhifadhi na ulinzi wa rasilimali za wanyamapori kwa muda mrefu na wamekuwa wakitupa mafuta, mahema na viona mbali "binoculars" amesema

Amesema Kanda ya Kaskazini inasimamia maeneo makubwa ambayo ni mikoa minne ya Manyara, Arusha, Tanga na Kilimanjaro ambayo yamekuwa yanakumbwa na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu hivyo kwa kupatiwa msaada huo hususani mahema yatawasaidia sana Askari kufanya kazi zao ipasavyo hasa kwa kazi za dharura zinazojitokeza mara kwa mara na kuwalazimu kwenda maeneo ambayo hayana vituo vya kudumu vya Askari.

Vilevile, ameiomba bodi hiyo kuendelea kuisaidia TAWA hususani Kanda hiyo kwakuwa wanasimamia maeneo makubwa yenye changamoto kubwa ya wanyamapori wakali na waharibifu na uhitaji bado ni mkubwa.

Post a Comment

0 Comments