Ticker

6/recent/ticker-posts

MRADI WA UJENZI WA SOKO JIPYA LA KARIAKOO WAFIKIA ASILIMIA 93%

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

MAENDELEO ya utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Soko jipya na ukarabati wa soko kuu la Kariakoo umefikia asilimia 93 na Mkandarasi amelipwa shilingi Bilioni 20 za utekelezaji wa mradi huo.

Ameyasema hayo leo Juni 27, 2024 Jijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja Mkuu wa Soko la kimataifa la Kariakoo Sigsibert Valentine wakati akizungumza na waandishi wa habari alipotembelea mradi huo na kujionea ulipofikia.

Amesema tayari Serikali imetoa shilingi Bilioni 28.03 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo unaolenga kutoa nafasi za biashara zipatazo 3,500 kwa watanzania pamoja na kutoa ajira zipatazo 4,000.

"Tunamshukuru Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mh. Albert Chalamila na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa ufafanuzi wanaoendelea kuutoa kwa umma kuhusiana na utekelezaji wa mradi na maandalizi ya kuwarejesha wafanyabiashara." Amesema

Aidha kuhusiana na kuwarejesha wafanyabiashara katika shughuli za biashara ameeleza kuwa, Shirika la masoko linautahadharisha Umma kuwa hakuna vizimba au maeneo mengine ya biashara yaliyogawiwa au kuuzwa kwenye soko hilo kama inavyodaiwa na baadhi ya wafanyabiashara.

"Nitoe wito kwa wananchi kuepukana na vishoka na kama kuna yeyote aliyeuziwa kizimba atoe taarifa kwenye vyombo husika." Ameongeza.

Pamoja na hayo amewataka wafanyabiashara kufuatilia taarifa kutoka katika Mamlaka husika ili kuepukana na vishoka walioanza kauwahadaa baadhi ya wafanyabiashara.

Amesema Shirika litaendelea kusimamia misingi yake ya uwazi na uwajibikaji kwa Umma kwa kuhakikisha inatoa taarifa sahihi na kwa wakati kwa wafanyabiashara kuhusu taratibu za upangishaji maeneo ya biashara muda utakapowadia.

Post a Comment

0 Comments