Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUIMARISHA USTAWI WA WATU WENYE UALBINO

Na; Mwandishi Wetu – Pwani

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuimarisha ustawi wa Watu wenye Ualbino nchini.

Amesema kuwa, katika utoaji wa huduma kwa Watu wenye Ulemavu wakiwemo wenye Ualbino, Serikali imehakikisha kundi hilo wanapata haki zao za msingi ikiwa ni pamoja na ustawi maisha yao.

Amesema hayo Jana (Alhamis Juni 13, 2024) katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya kukuza uelewa kuhusu Ualbino yaliyofanyika viwanja vya Maili Moja, Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Mkoani Pwani.

“Serikali imeendelea kuyapa kipaumbele masuala ya Watu wenye Ulemavu wakiwemo watu wenye ualbino, katika elimu, uwezeshwaji wa kiuchumi, ulinzi na usalama, afya, ajira, nyenzo za kujimudu pamoja na mafunzo ya ufundi stadi,” amesema

Kadhalika, ametoa rai kwa wadau mbalimbali kuendelee kushirikiana na Serikali katika kuwahudumia Watu wenye Ualbino.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Watu wenye Ulemavu, Rasheed Maftah amesema, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeanza maboresho ya Sera ya Huduma na Maendeleo kwa Watu wenye Ulemavu ya 2004, ambapo Sera hiyo inaandaliwa pamoja na mkakati wa utekelezaji ambao utajumiusha mahitaji ya mpango wa Watu wenye Ualbino.

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ualbino Tanzania (TAS), Godson Mollel ameishukuru Serikali kuanzisha mfumo wa kielektoniki wa kukusanya taarifa na takwimu za Watu wenye Ulemavu ambao utasaidia kuongeza ufanisi katika kuwatambua, kuwasajili na kuwaunganisha watu wenye ulemavu wakiwemo wenye Ualbino kupata huduma stahiki.

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya kukuza uelewa kuhusu Ualbino yameongozwa na kauli mbiu isemayo “Ushiriki, Ujumuishi na Ustawi”.

Post a Comment

0 Comments