Ticker

6/recent/ticker-posts

WANAHARAKATI WA JINSIA NA MAENDELEO WAICHAMBUA BAJETI YA MWAKA 2024/2025 KWENYE MLENGO WA JINSIA

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

WANAHARAKATI wa Jinsia na Maendeleo kupitia Mtandao wa Jinsia Tanzania- TGNP, wameishukuru Serikali kulifanyia kazi suala la kikokotoo ambacho kimeongezwa kutoka asilimia 33 hadi asilimia 40 ambapo kinatarajiwa kurejesha ahueni kwa wastaafu.

Akizungumza leo Juni 13,2024 Jijini Dar es salaam katika kijiwe cha kahawa kilichoandaliwa na TGNP -Mtandao kwa lengo la kufatilia bajeti iliyopitishwa ya mwaka 2024/2025, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi amesema licha ya serikali kuyafanyia kazi baadhi ya maeneo ambayo yamekuwa yakionekana yanachangamoto, kuna maeneo mengine bado hayafanyiwa kazi.

Amesema wanatamani kuona mradi wa SGR pamoja na  mradi wa bwawa la kuzalisha umeme ikisaidia watu wote  katika kujiendeleza kiuchumi yakiwemo makundi ya pembezoni kufaidika kwa kusafirisha mazao yao na kupata usafiri kwa urahisi ili waweze kujiendeleza kiuchumi.

"Tunavyozungumzia  mageuzi ya  kiuchumi,tuone sasa yale makundi ya pembezoni wale watu  ambao hawana uwezo wanawake,wanaume  maskini  na vijana wakiweza kufaidika kusafirisha mazao yao kupata usafiri kwa urahisi ili waweze kujiendeleza kiuchumi" amesema Lilian.

Aidha ameonesha shahuku yake kuhusiana na kuimarika kwa umeme nchini ambapo anatarajia kuona  wanawake na vijana wakikuza uchumi wao kwani umeme ni kichocheo cha ukuaji wa uchumi.

"Uchambuzi unahitajika kwa hii rasilimali iliyo wekezwa ambayo  tunajua ndio maana deni letu la taifa linakua  tuone sasa ina tija katika taifa letu" amesema.

Kwa Upande wake, Afisa wa Shirika la Wanawake katika Jitihada za Kimendeleo (WAJIK) Janeth Mawinza  amedai kuwa bajeti hiyo imewarudisha nyuma kama wanaharakati kwenda kujiandaa tena kwa sababu walivyoshauri havikubebwa kama walivyopendekeza hasa kuhusiana na suala la mlengo wa kijinsia pamoja na kulenga makundi maalumu.

"Tunatamani kama vyombo vyenye mamlaka vinaweza kufikiria na kujadili zaidi suala zima la elimu, tulitegemea tuone bajeti inasema elimu bure inaenda kupata nafasi ,watoto hawatakuwa na  michango shuleni" amesema

Naye,Mdau wa masuala ya kijinsia, Mophat Mapunda amepongeza kurudishwa kodi za ardhi na majengo katika mamlaka za halmashauri ambapo itazisaidia kujitanua kimapato katika vyanzo vya ndani  na kuchochea maendeleo.

Post a Comment

0 Comments