Ticker

6/recent/ticker-posts

KIJIJI CHA MNANILA BUHIGWE CHAPANDISHWA HADHI YA MJI MDOGO

Na Munir Shemweta, BUHIGWE

Kijiji cha Mnanila kilichopo tarafa ya Manyovu wilayani Buhigwe mkoani Kigoma kimepandishwa hadhi na kuwa mji mdogo ambapo sasa kijiji hicho kimewekewa mpango na kupimwa viwanja kwa lengo la kuharakisha maendeleo.

Uamuzi huo ni hatua ya utekelezaji vipaumbele vya wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ya Kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishaji wa ardhi mijini na vijijini

Hayo yamebainishwa jana na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda alipopewa fursa ya kuwasalimia wananchi wa kijiji cha Mnanila wakati wa ziara ya Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango mkoani Kigoma.

Amesema, kutokana na maendeleo yanayokuwa kwa kasi kwenye mji huo mdogo wa Mnanila, wizara yake imeona ipo haja ya kuupanga ili kuharakisha kasi ya maendeleo kwa wananchi.

"Tunataka kubadili sura ya kijiji kuwa mji mdogo ili mnufaike na mji huu. Tunataka manyanyuke magorofa anayetoka nchi jirani akifika aione tanzania yote iko manyovu". alisema Mhe.Pinda

Amebanisha kuwa, Wizara ya Ardhi inaenda kuweka mpango ili mji huo uwe katika mpangilio mzuri wa kimji utakaovutia sambamba na kuwa na maeneo yanayokidhi mahitaji ya wananchi wa mji huo.

"Wizara tayari tumeshaanza kuuweka mji katika mpango na tumepima takriban viwanja 1000 na maelekezo yangu mpango huu lazima uwe shirikishi " amesema Mhe. Pinda.

Amemuelekeza Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Kigoma Palmon Martin Rwegoshora kuhakikisha wakati wa urasimishaji makazi holela wananchi wanashirikishwa ili kuondoa migongano inayoweza kujitokeza.

"Wananchi washirikishwe kuanzia hatua za awali na elimu itolewe ili wajue mji unaofikiriwa kupelekwa utakuwa wa namna gani lakini vinginevyo tayari tushahamisha kwenye level ya kijiji kuwa mji mdogo kwa sababu ya mapokeo yanayoenda kufanyika. ". Alisema Mhe. Pinda

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, mji huo mdogo wa Mnanila unaoenda kujengwa pia Kituo kikubwa na cha kisasa cha forodha ni vizuri ukaendana na miji mingine yenye vituo hivyo na wananchi wanatakiwa kuyapokea mabadiliko yanayoenda kuubadilisha mji huo.

Kufuatia mpango wa uendelezaji katika mji mdogo wa Mnanila, Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Kigoma Palmon Rwegoshora ameeleza kuwa, tayari michoro ya mipango miji imeandaliwa na kupatikana takriban viwanja 1000 upande wa kuelekea mpaka wa Tanzania na Burundi.



" Michoro ya mipango miji katika mji huu mdogo wa Mnanila imeandaliwa na tayari vimepatikana takriban viwanja 1000 kuelekea border ya Burundi na zoezi linaloenda kufanyika ni urasimishaji kwenye maeneo yenye makazi holela na zoezi hilo litakuwa shirikishi" alisema Rwegoshora.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akizungumza na wananchi wa Buhigwe mkoani Kigoma alipopewa fursa ya kuwasalimia wakati wa ziara ya Makamu wa Rais Mhe. Dkt Philip Mpango jana.
Sehemu ya wananchi wa Mji mdogo wa Mnanila wilayani Buhigwe waliojitokeza kumlaki Makamu wa Rais Mhe. Dkt Philip Mpango wakati wa ziara yake mkoani Kigoma jana.
Makamu wa Rais Mhe. Philip Mpango akisalimiana na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda alipowasili kukagua mradi wa ujenzi wa hospitali ya kanda ya magharibi pamoja na kampasi ya chuo kikuu kishiriki cha afya muhimbili kanda hiyo wakati wa ziara yake mkoani humo jana. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Post a Comment

0 Comments