Ticker

6/recent/ticker-posts

PINDA AMREJESHEA NYUMBA BIBI ALIYOIHANGAIKIA KWA ZAIDI YA MIAKA 10 KIGOMA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amemrejeshea nyumba Bi Leticia Benedict Choma mwenye umri wa zaidi ya miaka 80 mkazi wa Kigoma Ujiji baada ya kuihangaikia kwa zaidi ya miaka 10 bila mafanikio.

Bi. Leticia Choma anadaiwa kudhulumiwa nyumba aliyoachiwa na marehemu baba yake Bw. Benedict Choma iliyopo eneo la Mwanga barabara ya Bibi Titi Kigoma Ujiji kama urithi baada ya nyumba hiyo kuuzwa na msimamizi bandia wa mirathi asiyeidhinishwa na mahakama kwa madai ya kutokuwa na haki ya kumiliki nyumba hiyo licha ya wazazi wake kujenga na yeye kuzaliwa na kuishi hapo kwa miaka yote.

Kwa mujibu wa Bw. John Benedict Matata aliyemsimamia Bi. Leticia, mgogoro wa nyumba hiyo ulianza mwaka 2010 pale walipoanza kufuatilia kuhuisha hati ya nyumba hiyo Plot Na 212 Kitalu M mtaa wa Mwanga Kigoma Ujiji yenye namba ya usajili 13176 iliyokwisha muda wake mwaka 1989. kuisha kwa muda wa hati hakumkoseshi haki mmiliki ingawa Bi. Leticia amekuwa akizungushwa kwa miaka yote.

Amefafanua kuwa, pamoja na juhudi walizofanya ikiwemo kupita taasisi na mamlaka tofauti kutafuta kwa lengo la kutafuta haki lakini hawakuweza kufanikiwa hadi walipopata fursa ya kukutana na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda wakati wa ziara ya Makamu wa Rais mkoani Kigoma.

Ameeleza kuwa, katika kutafuta suluhu ya suala hilo Mhe Pinda aliwasikiliza kwa makini na baadaye kuitisha kikao cha pamoja kati ya Mwakilishi wa Kamishna wa Ardhi nchini, Msajili wa Hati na Nyaraka mkoa wa Kigoma pamoja na Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa.

Bw. Matata ameweka wazi kuwa, kutokana na nyaraka walizokuwa nazo za umiliki wa nyumba yenye mgogoro na maelezo ya Bi. Leticia kuhusiana na sakata hilo pande zote zilikubaliana pasipo shaka kuwa, Bi Leticia Choma ndiye mmiliki halali wa nyumba hiyo.

"Baada ya kufuatilia kwa muda mrefu Mwenyezi Mungu amemleta kiongozi Mhe. Pinda, Mungu amzidishie maisha marefu ndiyo tumepata msaada huu leo kuja kumletea malalamiko na namshukuru sana Mheshimiwa’’ alisema Matata.

Kwa upande wake Mhe. Geophrey Pinda ameagiza Bibi Leticia Choma kutobughudhiwa na mtu yeyote baada ya kurejeshewa nyumba yake huku akimtaka Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Kigoma kulisimamia suala hilo.

‘’Hakuna wa kuingilia tena kuleta shida, huyu bibi asibughudhiwe na wale wote wanaoendesha dhulma kama hii tutakufa nao’’ alisema Mhe. Pinda
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akimkabidhi Hati Milki ya Ardhi Bi. Leticia Choma aliyetaka kudhulumiwa nyumba ya urithi wa baba yake iliyopo Barabara ya Bibi Titi eneo la Mwanga Kigoma Ujiji. Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akisisitiza jambo kwa Bw. John Matata (kulia) kuhusiana na hati aliyomkabidhi Bi Leticia Choma aliyetaka kudhulumiwa nyumba ya urithi wa baba yake mkoani Kigoma.Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akizungumza na Bi. Leticia Choma aliyetaka kudhulumiwa nyumba ya urithi wa baba yake iliyopo Barabara ya Bibi Titi eneo la Mwanga Kigoma Ujiji mkoani Kigoma. Bi Leticia Choma (aliyeshikwa mkono) akitoka ofisi za Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Kigoma mara baada ya kukabidhiwa hati ya nyumba yake ya urithi wa baba yake mzazi na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda.Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda akiwa na maafisa wa Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Kigoma wakati akimkabidhi hati milki ya ardhi Bi Letecia Choma aliyetaka kudhulumiwa nyumba ya urithi wa baba yake mkoani Kigoma. (PICHA NA WIZARA YA ARDHI)

Post a Comment

0 Comments