WAZAZI na walezi wametakiwa kuwa na aina au mfumo wa malezi ya Kidemokrasia ikiwemo kujenga mahusiano mazuri pamoja na kutilia maanani hisia za mtoto au watoto.
Wito huo umetolewa leo Julai 3, 2024 katika Semina za Jinisa na Maendeleo ambazo hufanyika kila Jumatano katika Viwanja vya TGNP- Mtandao Mabibo Jijini Dar es Salaam.
Mwanasaikolojia Sylvia Sostenes wakati akiwasilisha mada kuhusu malezi, amewasihi walezi wote kuwa na muda wa kutosha wa kukaa na watoto wao kama nyenzo ya kufuatilia mwenendo wa mtoto au watoto.
Mwanasaikolojia
huyo ameendelea kwa kufafanua kuwa, kulea ni pamoja na kuwekeza katika
mahitaji muhimu kama lishe bora, afya ya mwili, roho na akili, elimu,
ulinzi, muda kwa ajili ya kuchangamana na watoto.
Katika uwanda
wa kisaikolojia, Bi. Sylvia ameeleza kuwa, malezi ni mchakato
uliosheheni vitu vingi ndani yake lakini kubwa zaidi ikiwemo na kumpatia
mtoto mahitaji yake na huduma muhimu.
"Malezi ni mchakato wa
maandalizi ya mtoto utakaomwezesha mtoto kukua, kukubalika, kujikubali,
kushiriki katika shughuli za kijamii na kiutamaduni kwa kumlinda,
kumjumuisha na kumpatia mahitaji na huduma za msingi" alisema Bi. Sylvia
na kuongeza kuwa
"Iwapo malezi ni mchakato wa maandalizi ya
mtoto basi sharti iwepo mikakati toka kwa wazazi/walezi ili kufanikisha
hili. Kwasasa tunaishi kwenye huu mtindo huria ambao ni wa kujipatia
Watoto na kuwaacha wakue. Watoto wanajilea wao wenyewe."
Akichangia
katika semina hiyo, Joseph Bulemo amesema kwa sasa, familia nyingi
hazina ukaribu na watoto jambo linalopelekea matukio ya ukatili kwa
watoto kuendelea kutokea.
Bw. Bulemo pia ameyataja malezi ya kimabavu dhidi ya watoto kama sababu inayopelekea watoto kuwa karibu na wazazi au walezi.
Naye
Nantaika Maufi amashauri wazazi kuwa karibu na watoto katika kila hatua
kwani kwa kufanya hivyo itawasaidia kugundua mapema mabadiliko yoyote
au pindi watoto wapatapo changamoto yoyote au kufanyiwa ukatili huku
akipinga hoja ya ugumu wa maisha na shughuli za utafutaji kama kikwazo
cha kutokuwa karibu.
Kwa upande wake Mpegwa Noah amewataka wazazi
na walezi kuwa na umoja wa dhati na uchungu sawa kwenye malezi kwa
watoto wao, watoto wa majirani na watoto wengine wowote kwa kufanya
hivyo itachangia watoto katika maadili mazuri kwa kuoata malezi bora.
0 Comments