Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI KIJAJI ATEMBELEA KITUO CHA TAIFA CHA UFUATILIAJI WA KABONI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Ashatu Kijaji amezitaka Taasisi za Elimu ya Juu nchini kuandaa na kuzalisha wataalamu watakaosaidia kubuni na kubaini fursa zitokanazo na uhifadhi wa mazingira ikiwemo biashara ya kaboni.

Dkt. Kijaji amesema hayo Julai 9, 2024 Mkoani Morogoro wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni kwa ajili ya kujitambulisha na kufahamu majukumu mbalimbali ya kiutendaji ya kituo hicho.

Amesema suala la uhifadhi wa mazingira kwa sasa limepata mwitikio na mwamko mkubwa kutoka kwa wananchi walio wengi, hivyo nafasi hiyo haina budi kutumika vyema na wataalamu kubuni mbinu rafiki na wezeshi zenye kuibua zilizopo katika upandaji miti na uhifadhi wa misitu.

“Ushirikiano baina ya Serikali na taasisi za elimu ya juu ni muhimu kwani itahamasisha wananchi kuhifadhi mazingira, tuandae wataalamu kuanzia ngazi ya cheti ili kuwaelimisha wananchi manufaa na faida za upandaji miti na utunzaji wa misitu” amesema Dkt. Kijaji.

Aidha Dkt. Kijaji amesema elimu ya uhifadhi wa mazingira ikitolewa kwa wananchi itasaidia katika ukuaji wa sekta za kijamii na kiuchumi ikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi n.k kwa kuwa shughuli hizo zitaendeshwa kwa kuzingatia miongozo ya kitalaamu na kuwaletea faida.

Ameongeza kuwa wakati umefika kwa wataalamu kujitokeza na kuandaa mikakati ya pamoja itakayosaidia wananchi kunufaika na fursa mbalimbali zitokanazo na rasimali na sekta za misitu na mazingira ikiwemo uwepo biashara ya kaboni ambayo kwa kiwango kikubwa inatokana na upandaji miti.

“Tuwaelimishe wananchi ili waone manufaa ya upandaji miti kwa kuhakikisha wanaachana na shughuli zisizo endelevu kwa mazingira ikiwemo ukataji miti kwa ajili ya kuni…Juhudi za pamoja zinahitajika ili wananchi waweze kunufaika na uhifadhi wa mazingira hususani biashara ya kaboni” amesema Dkt. Kijaji.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni, Prof. Eliakimu Zahabu amesema biashara ya kaboni ni mfumo uliopo katika soko la dunia unaohusisha upandaji na utunzaji wa miti inayodhibiti uzalishaji wa hewa ukaa katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, nishati, viwanda, na miundombinu.

“Katika kukabiliana na mabadiliko tabianchi, Dunia imeiona haja ya kuendesha biashara ya kaboni..Tumeendelea kutoa elimu kwa jamii na tumeshuhudia wananchi wa Halmashauri mbalimbali nchini wakipata faida ikiwemo miradi ya maendeleo na fedha” amesema Prof. Zahabu.

Naye Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Kemilembe Mutasa amesema Tanzania ni miongoni mwa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa zilizoridhia Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi unaosisitiza umuhimu wa kuweka wa jitihada za pamoja za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ameongeza kuwa jitihada hizo zimeibua changamoto na fursa mbalimbali zinazosaidia kuchochea shughuli endelevu za uhifadhi wa mazingira ikiwemo uratibu wa biashara ya Kaboni ambayo inalenga kupunguza uzalishaji wa gesijoto duniani.

“Katika kuhakikisha changamoto za mabadiliko ya tabianchi zinakuwa na manufaa na matokeo chanya, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja kufanya mapitio ya sera, uandaaji wa kanuni, mikakati na miongozo inayolenga kuweka mazingira rafiki ya usimamizi wa mazingira” amesema Kemilembe.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Watalaamu mbalimbali kutoka Chuo Kikuu cha Sokoino cha Kilimo (SUA), baadhi ya wajumbe wa menejimenti ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Watendaji Waandamizi wa Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC).
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (mbele) akifurahia jambo na Viongozi mbalimbali wa Ofisi hiyo akiwemo Mkurugenzi wa Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) Prof. Eliakimu Zahabu (kushoto) na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi wa pili (kushoto) muda mfupi baada ya kuwasili katika Ofisi za Kituo cha NCMC zilizopo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Julai 9, 2024 Mkoani Morogoro.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (mbele) akisaini kitabu cha wageni muda mfupi baada ya kupokelewa na mwenyeji wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Maulid Mwatawala (hayupo pichani) Chuoni hapo Julai 9, 2024 Mkoani Morogoro. Kulia ni Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Ashatu Kijaji (kulia) akizungumza jambo wakati wa kujitambulisha kwake kwa Uongozi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wakati wa ziara yake ya kutembelea Kituo cha Taifa cha Biashara ya Kaboni (NCMC) Julai 9, 2024 Mkoani Morogoro. Katikati ni Naibu Makamu Mkuu wa SUA, Prof. Maulid Mwatawala na kushoto ni Mkurugenzi wa Kituo cha NCMC, Prof. Eliakimu Zahabu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Ashatu Kijaji (kulia) akizungumza jambo wakati wa kujitambulisha kwake kwa Uongozi wa wakati wa ziara yake ya kutembelea Kituo cha Taifa cha Biashara ya Kaboni (NCMC) Julai 9, 2024 Mkoani Morogoro. Kushoto ni Makamu Mkuu wa SUA, Prof. Maulid Mwatawala.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Maulid Mwatawala (kushoto) akizungumza jambo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Ashatu Kijaji (kulia) akizungumza jambo wakati wa ziara ya Mhe. Kijaji kutembelea Kituo cha Taifa cha Biashara ya Kaboni (NCMC) Julai 9, 2024 Mkoani Morogoro.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Ashatu Kijaji akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Makamu MkuU wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Maulid Mwatawala muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao baina yao Chuo hapo Julai 9, 2024 wakati wa ziara yake ya kutembelea Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC). Wa kwanza kulia ni Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (kulia) akizungumza jambo na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Maulid Mwatawala muda mfupi baada ya kumalizika kwa mazungumzo baina yao Chuo hapo Julai 9, 2024 wakati wa ziara yake ya kutembelea Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC).
Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi akizungumza jambo wakati alipokuwa akitoa maelezo ya awali kuhusu kituo cha taifa cha ufuatiliaji wa kaboni kwa Mhe. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Ashatu Kijaji (katikati) wakati wa ziara yake katika kituo hicho Julai 9, 2024 Mkoani Morogoro. Kushoto ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Maulid Mwatawala.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Maulid Mwatawala akizungumza jambo wakati wa ziara ya Mhe. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Ashatu Kijaji (katikati) katika Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) Julai 9, 2024.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza jambo wakati wa ziara yake aliyoifanya katika Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Biashara ya Kaboni (NCMC) kilichapo Mkoani Morogoro Julai 9, 2024. Kulia ni Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi na kushoto ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Maulid Mwatawala.

(PICHA NA MPIGAPICHA WETU)

Post a Comment

0 Comments