Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, Mhe. Dkt. Jasson Rweikiza (Kushoto) akifuatilia wasilisho la Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Patrobas Katambi, kuhusu utekelezaji wa maagizo ya Kamati hiyo yaliyotolewa Oktoba 2023.
Na Mwandishi Wetu
Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umewasilisha maboresho ambayo yamefanyika katika kanuni mbili za usalama na afya mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo.
Maboresho hayo ambayo yamefanyika katika kanuni za Igonomia na Mazingira ya Kazi yalishauriwa kufanyika na Kamati hiyo katika kikao chake cha Oktoba 26, 2023 baada ya OSHA kuwasilisha kanuni hizo mpya mbele ya Kamati hiyo.
Wasilisho hilo limefanywa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi, ambaye alimwakilisha Waziri wake Mhe. Ridhiwani Kikwete. Katambi ameambatana na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, Kamishna wa Kazi, Bi. Suzan Mkangwa na Watendaji wengine wa Wizara na Taasisi ya OSHA.
Mhe. Katambi ameiambia Kamati kuwa mapendekezo yote yaliyotolewa ikiwemo kujumuisha tafsiri ya neno Mamlaka pamoja kuondoa maudhui yanayojirudia katika kanuni hizo yameshughulikiwa ipasavyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Dkt. Jasson Rweikiza, ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) pamoja na Taasisi ya OSHA kwa kupokea na kutekeleza maagizo ya Kamati yake.
Aidha, ameahidi Kamati yake kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi chini yake katika kuwahudumia Watanzania kupitia ushauri na maelekezo mbalimbali yanayolenga kuboresha utendaji wa Serikali.
Wakati huo huo, OSHA imekutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na kufanya wasilisho kuhusu utendaji wa Taasisi hiyo ambapo Mtendaji Mkuu, Bi. Khadija Mwenda, ameieleza Kamati hiyo umuhimu wa kulinda nguvukazi ya Taifa kupitia uimarishaji wa mifumo ya usalama na afya katika sehemu za kazi.
“Hadi inapofika hatua ya mtu kuajiriwa kama mfanyakazi serikali inakuwa imewekeza rasilimali nyingi sana kwake kuanzia anapozaliwa, kukua, kusoma hadi kuajiriwa hivyo inakuwa ni hasara kubwa kwa Taifa endapo mfanyakazi huyu atapata ulemavu au kupoteza maisha kabla ya kutoa mchango wake wa kutosha katika uzalishaji,” ameeleza Mtendaji Mkuu wa OSHA na kuongeza:
“Tunachokifanya OSHA ni kushauri na kusimamia maeneo ya kazi kuweka mifumo madhubuti ya kuwalinda wafanyakazi dhidi ya vihatarishi vya magonjwa pamoja na kulinda mitaji ya wawekezaji ili kuleta tija katika uzalishaji pamoja na kulinda ustawi wa wafanyakazi.”
Akihitimisha mjadala wa wajumbe wa Kamati hiyo ya Bajeti baada ya wasilisho la OSHA, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Oran Njeza, amesema Kamati yake itaendelea kutoa ushauri unaolenga kuboresha utendaji wa Serikali ikiwemo Taasisi ya OSHA.
Mjadala ukiendelea katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo ambapo OSHA iliwasilisha maboresho ya kanuni mbili za usalama na afya.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi, akifanya wasilisho mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu maboresho ya kanuni za Igonomia na Mazingira ya Kazi ambayo Kamati hiyo ilielekeza yafanyike.
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda na Kamishna wa Kazi, Bi. Suzan Mkangwa wakifuatilia wasilisho la Naibu Waziri, Mhe. Katambi katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria NdogoWatendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) na Taasisi ya OSHA wakifuatilia wasilisho la Naibu Waziri, Mhe. Katambi katika kikao cha Kamati ya ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo.
0 Comments