Ticker

6/recent/ticker-posts

MKURUGENZI MKUU REA AHAMASISHA WANANCHI KUTUMIA NISHATI SAFI YA KUPIKIA


Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy amewaasa wananchi kutumia Nishati Safi ya Kupikia ili kuokoa gharama na muda, kulinda mazingira na afya zao hasa ikizingatiwa kuwa teknolojia sasa imeboreshwa na gharama yake ni ndogo ikilinganishwa na nishati zingine.

Mhandisi Saidy ametoa rai hiyo Agosti 8, 2024 mbele ya wananchi waliotembelea Banda la REA katika Maonesho ya Siku Kuu ya Wakulima (Nane Nane), Nzuguni Jijini Dodoma.

"Tunaendelea kuhamasisha wananchi kutumia Nishati Safi ya Kupikia kwani ni salama, rafiki na gharama yake ni nafuu kwani teknolojia sasa imeboreshwa," amesema Mhandisi Saidy.

Mhandisi Saidy amesema ipo dhana ambayo imejengeka katika jamii kuwa matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ni ghali na si salama na pia chakula kinachopikwa kutokana nayo hakina ladha suala ambalo alisisitiza si kweli.

"Ninawathibitishia Nishati Safi ya Kupikia ni salama kuliko nishati zingine tulizozizoea, niwatoe wasiwasi katika hili na tunaendelea kutoa elimu kuhusu usalama na umuhimu wa nishati hii bora," amesema Mhandisi Saidy.

Akizungumzia upatikanaji wa Nishati Safi ya Kupikia kwa wote, amesema Serikali imetoa ruzuku katika usambazaji wa Mitungi ya Gesi (LPG) na Majiko Banifu ili kuvutia wawekezaji wengi na pia kumuwezesha kila mwananchi aweze kumudu gharama zake.

"Serikali imekuja na mfumo wa kumrahisishia kila mwananchi hususan yule mwenye kipato cha chini kumudu gharama ya Nishati Safi ya Kupikia kokote aliko ili aachane na matumizi ya nishati nyingine," amefafanua Mhandisi Saidy.

Amesema Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameipatia REA jukumu la kuhakikisha inasimamia vyema utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034 ili kufikia 2034 asilimia 80 ya wananchi wawe wanatumia Nishati Safi ya Kupikia.

"Tunamshukuru Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuamini na kutupatia jukumu hilo kubwa na tayari kwa kushirikiana na wadau tumeanza utekelezaji wake na tunakwenda vizuri," amefafanua Mhandisi Saidy.

Amesema hatua inayoendelea sasa ni kuibua na kuwawezesha wazalishaji wengi wa vifaa vya Nishati Safi ya Kupikia ili kuongeza umahiri sambamba na kuwawezesha kutengeneza bidhaa nyingi kwa gharama nafuu na kwa ubora wa kimataifa," amesema.

Amesema kwa kufanya hivyo kutakuwa na ongezeko la matumizi ya nishati safi ya kupikia, ongezeko la ajira na hivyo kukuwa kwa uchumi.

Post a Comment

0 Comments