Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI- HAKUNA MWANANCHI ANAYEONDOLEWA NGORONGORO KWA AJILI YA UTALII BALI UHIFADHI


NA MWANDISHI WETU

Serikali imesema uhamisho unaoendelea wa wananchi waishio ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ni wa hiari baada ya wananchi husika kupewa Elimu, kuhamasika na kuridhia wenyewe kwenda Msomera na maeneo mengine waliochagua kupisha uhifadhi wa raslimali kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo siyo utalii.

Mkurugenzi wa Idara ya Wanyapori nchini, Dkt. Alex Lobora amefafanuakwamba kuhama kwa hiari kwa wananchi ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) kunatokana na tathmini shirikishi iliyofanyika mwaka 2020 na siyo upotoshwaji unaoenezwa na baadhi ya vikundi vya watu wenye nia ovu.

“Tathmini hiyo ilionesha kuwa shughuli za kibinadamu zinazoendelea ndani ya eneo hilo siyo rafiki kwa maisha ya binadamu na ni hatarishi kwa binadamu wenyewe na uhifadhi.” Amesisitiza Dkt. Lobora .

Ameongeza kuwa pamoja na kutokuwa na mazingira rafiki kwa maisha na maendeleo ya binadamu, eneo la Ngorongoro limehifadhiwa kwa sheria Sura Na.284 ambayo hairuhusu baadhi ya maendelezo kwa mustakabali wa kulinda na kuhifadhi maliasili na malikale zilizomo katika eneo hilo ambazo siyo tu ni muhimu kwa Tanzania bali dunia nzima na kwamba eneohilo ni la urithi wa dunia.

Kuhusu madai ya baadhi ya wananchi hususan wamasai kuwa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kuwa ni eneo lao la mababu (ancestral land) na kwamba wao ni watu wa asili (indigenous people) wa eneo hilo hayana msingi wowote na ni upotoshaji wa ukweli na unaolenga kuwatofautisha wananchi wa eneo hilo na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye nia njema kwa watu wake.

Ameeleza kuwa katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro yapo makabila mengine kama Wadzabe na wadatoga ambao walitangulia kuishi NCA kabla hata ya jamii ya Wamasai.

“Kwa mujibu wa Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) Sehemu ya 15 na 17 vinatoa uhuru wa watu na uhuru wa kuwa mahali popote na hakuna ubaguzi chini ya Sehemu ya 13 ya Katiba. Tanzania haina watu wa asili bali watu wote ni sawa na wanaruhusiwa kuishi mahali popote ilimradi wasivunje Sheria. Aidha, Sheria ya Ardhi Na. 4 ya Mwaka 1999 inafafanua kuwa Tanzania ina aina tatu tu za ardhi (Ardhi Iliyohifadhiwa, Ardhi ya Kijiji na Ardhi ya Jumla). Hakuna “ancestral land”. Amesisitiza Dkt. Lobora. 

Amefafanua kuwa yako madhara mengi kwa wananchi waishio ndani ya NCA ambayo yanawafanya kupingana na “Millennium Goals” zinazoeleza hali inayotakiwa kwa mtu anayetakiwa kuitwa binadamu ikiwemo kukosa haki ya kumiliki ardhi na kukosa huduma nyingine za msingi ambazo haziwezi kupatikana ndani ya eneo lililohifadhiwa kwa mujibu wa Sheria.

Aidha amesema wananchi wanaohamia Msomera na maeneo mengi kwa hiari wananufaika na mambo mengi wanayopatiwa na serikali ambapo ametaja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na kupewa fidia ya maendelezo na motisha ikiwa ni hatua ya Serikali kuwaokoa kutoka kwenye maisha duni yasiyo na matumaini na kuboresha maisha yao.

Post a Comment

0 Comments