Na Mwandishi Wetu, Mbeya
Maofisa wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wametembelea na kutoa elimu kwa wajasiriamali wanaoshiriki Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayofanyika kwenye Viwanja vya John Mwakangale mkoani Mbeya na kuwapatia elimu ili waweze kufika TBS kupata alama ya ubora.
Aidha, Shirika hilo limetumia maonesho hayo kutoa elimu ya masuala ya viwango kwa wananchi ili waweze kuondokana na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo, ikiwa ni pamoja na namna ya kutambua bidhaa zilizoisha muda wake wa matumizi pamoja na vipodozi vyenye viambata sumu ambavyo vimepigwa marufuku kwenye soko la Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari leo kwenye Viwanja vya John Mwakangale Meneja wa TBS Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Abel Mwakasonda, alisema tangu kuanza kwa maonesho hayo ya Nanenane Agosti 1, mwaka huu imekuwa ni fursa nzuri kwa shirika kutembelea wajasiriamali na kuwapatia elimu kuhusu masuala ya viwango.
Alisema mbali ya kutoa elimu kuhusu namna ya kupata alama ya ubora, wamehimiza wajasiriamali kutumia fursa iliyotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kuthibitisha bora wa bidhaa zao bure, kwani gharama hizo zinalipwa na Serikali.
"Serikali kwa kutambua mchango wa wajasiriamali katika kukuza uchumi wa nchi, imeamua kubeba gharama zote kwa kuthibitisha ubora wa bidhaa za wajasiriamali, kwani hiyo wanachotakiwa ni kuja TBS wakiwa na barua ya utambulisho kutoka SIDO na sisi bila kuchelewa tutaanza mchakato wa kuthibitisha bidhaa zao na kuwapa alama ya ubora," alisema Mwakasonda.
Alisema wajasiriamali hawana sababu ya kuogopa kwa kudhani kuthibitisha bidhaa ni gharama, kwani Serikali chini ya Rais Samia inatambua mchango wao, ndiyo maana imeamua kubeba jukumu hilo," alisema Mwakasonda.
Alitaja faida bidhaa kuwa na alama ya ubora ya TBS kuwa ni pamoja na kuwawezesha wazalishaji kuingia kifua mbele kwenye soko, kwani bidhaa zao zinakuwa zinaaminika na hakuna mtu mlaji anayeweza kuzitilia shaka.
Aidha, alisema mbali na bidhaa hizo kukubalika kwenye soko, wazalishaji wataweza kuuza bidhaa hizo katika nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) bila kikwazo chochote.
Kwa mujibu wa Mwakasonda nchi zote wanachama wa EAC zimeingia makubaliano, ambapo bidhaa zikishapimwa na kuthibitishwa ubora na shirika la viwango la nchi husika, zinaruhusiwa kuingia nchi yoyote bila kutakiwa kupimwa tena.
"Hii ni fursa kubwa kwa Watanzania ndiyo maana tupo hapa tangu tarehe moja kwa ajili ya kutoa elimu kwa wajasiriamali na wazalishaji kwa ujumla, kwani Serikali yao haitaki kumuacha nyuma hata mmoja," alisema Mwakasonda na kuongeza;
Kwa upande wa wananchi, Mwakasonda alisema waliofika kwenye maonesho hayo walipata elimu kuhusu namna ya kutambua bidhaa ambazo zimeisha muda wake wa matumizi, ambapo alihimiza Watanzania kujenga utamaduni wa kusoma taarifa zilizopo kwenye vifungashio.
Alisema matumizi ya bidhaa ambazo zimeisha muda wake yana madhara kiafya. Aidha aliwahimiza kuhakikisha bidhaa wanazonunua zina alama ya ubora wa TBS. Maonesho hayo yalifunguliwa Agosti 2, mwaka huu na yatanalizika tarehe 08.
0 Comments