Ticker

6/recent/ticker-posts

WADAU WA AFYA WA KANDA WATAKIWA KUJADILI MBINU ZA KUIMARISHA MIFUMO YA AFYA NCHINI

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema nchi wanachama ikiwemo Tanzania zimejitahidi kuwekeza katika sekta ya afya na kupunguza gharama za kupeleka wagonjwa nje ya Kanda kwa matibabu.

Ameyasema hayo leo Agosti 30, 2024 katika Mkutano wa 12 wa Shirikisho la Watoa Huduma za Afya Afrika Mashariki uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Njerere (JNICC). Dar es Salaam

Aidha Majaliwa ametoa wito kwa wawekezaji wa Sekta ya Afya kuwekeza nchini Tanzania kwa kuwa Serikali imetengeneza sera rafiki za uwekezaji hususan katika Sekta ya Afya kutokana na uhitaji wa huduma hizo nchini.

"Tunawakaribisha wawekezaji wote wenye nia ya kuwekeza kwenye sekta ya afya, Sera nzuri tunazo, Sheria na kanuni nzuri tunazo, mahitaji ya uwekezaji kwenye sekta ya afya ni makubwa na tunataka tupate teknolojia mpya na huduma za kibingwa."

Pamoja na hayo amewataka wadau wa afya wa kanda kujadili mbinu mbalimbali za kuimarisha mifumo ya afya na kuwa na mikakati ya pamoja ya kukabiliana na magonjwa.

"Tumieni jukwaa hili kuweka mikakati ya pamoja ya kupambana na magonjwa ya mlipuko, magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ambukiza pamoja na magonjwa mapya yanayotokana na mabadiliko ya hali ya tabia nchi". Amesema Majaliwa .

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema kwa sasa ni wagonjwa wachache wanaosafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu, kwani karibu magonjwa yote makubwa sasa yanaweza kutibiwa ndani ya Afrika Mashariki.

Amesema uwekezaji uliofanywa na serikali kuanzia ngazi ya chini umewezesha ugunduaji wa magonjwa yakiwa katika hatua za awali.

"Rufaa kwenda nje ya Nchi zimepungua kwa kiasi kikubwa kipindi cha nyuma watu waliokuwa wanafika Ocean road walikuwa kwenye hatua za mwisho za ugonjwa, lakini kutokana na uwekezaji sasa zaidi ya asilimia 70 ya wagonjwa wanakuja wakiwa na magonjwa katika hatua za awali" Amesema Dkt. Mollel 

Post a Comment

0 Comments